Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Rekodi dabi za Agosti

Dabi Pic Data Rekodi dabi za Agosti

Thu, 8 Aug 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Mechi ya lawama imefika. Ndio, watani wa jadi wa soka nchini, Simba na Yanga kesho Alhamisi watashuka uwanjani kumalizana katika pambano la Ngao ya Jamii, kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam baada ya wikiendi iliyopita kutesti mitambo katika matamasha ya klabu hizo kongwe yaliyofana.

Simba ilifanya tamasha la 16 la Simba Day Jumamosi iliyopita na kutambulisha kikosi kipya cha msimu wa 2024-25 kabla ya kupata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya APR ya Rwanda, kisha siku iliyofuata Yanga ilijibu mapigo kwenye Kilele cha Wiki ya Mwananchi kwa kuinyoosha 2-1 Red Arrows ya Zambia.

Tangu mechi hizo mbili na baada ya mashabiki na wapenzi kuviona vikosi vyote viwili, kumekuwa na tambo nyingi kabla ya pambano hilo la nusu fainali ya Ngao ya Jamii inayoashiria kuzinduliwa kwa msimu mpya, ambao utatanguliwa na mechi nyingine kati ya Azam FC na Coastal Union zinazovaana visiwani Zanzibar.

Hii ni mechi ya 17 kwa vigogo hivyo kukutana ndani ya Agosti katika mechi za mashindano yote, huku rekodi zikiibeba Yanga iliyoshinda nane, Simba ikishinda saba na sare 2.

Simba ndio watetezi wa taji hilo walilolitwaa msimu uliopita ndani ya mwezi huo kwa ushindi wa penalti 3-1 baada ya muda wa kawaida kuisha kwa suluhu.

Mwanaspoti linakuletea orodha ya mechi zote za Dabi ya Kariakoo zilizopigwa Agosti. Tiririka nayo...!

LIGI KUU TANGU

Timu hizo zilikutana kwa mara ya kwanza katika pambano la kihistoria lililopigwa Nyamagana, Mwanza ikiwa ni mechi ya 10 kwa watani tangu kuasisiwa kwa Ligi ya Bara mwaka 1965.

Mechi hiyo ilipigwa Jumamosi ya Agosti 10, 1974 na vijana wa Jangwani waliibuka na ushindi wa mabao 2-1 kupitia mabao ya Gibson Sembuli dk. 87, Sunday Manara dk. 97, huku Wekundu wa Msimbazi wakitangulia mapema kwa bao la dakika ya 16 la Adam Sabu.

Mechi ya pili kwa timu hizo kukutana Agosti katika Ligi ilikuwa ni miaka 11 baadaye ambapo mechi ilipigwa Agosti 10, 1985 na Yanga kushinda tena kwa mabao 2-0.

Miezi michache baadaye timu hizo zilikutana tena katika Ligi Agosti 23, 1986 na safari hii Simba ilijibu mapigo kwa kushinda mabao 2-1 yaliyowekwa kimiani na Edward Chumila (dk9) na Malota Soma aliyefunga (dk51), licha ya Yanga kutangulia mapema kupata bao kupitia kwa Omary Hussein ‘Keegan’.

Mechi ya nne kwa timu hizo kukutana ilikuwa ni Agosti 15, 1987 na Yanga kushinda kwa bao 1-0 lililowekwa kimiani na Abeid Mziba ‘Tekelo’ (dk14).

SCUD YAILIPUA MSIMBAZI

Baada ya kupita ya kupita miaka minne tangu timu hizo kukutana Agosti, mwaka 1991 Dabi ya Kariakoo ilipigwa tena ndani ya mwezi huo na kama kawaida, Yanga ilishinda tena kwa bao 1-0 na kuendeleza rekodi nzuri.

Safari hii mechi ilipigwa Jumamosi ya Agosti 31 na Said Swedi ‘Scud’ aliyekuwa nyota mpya aliilipua Simba kwa bao pekee, akiendelea kismati cha kuifunga nje ndani Simba katika msimu huo.

Mwaka mmoja baadaye timu hizo zilikutana tena Agosti 31, lakini ikiwa ni mwaka 1997. Dakika 90 ziliisha bila kupatikana mbabe kutokana na kutoka suluhu, lakini miaka miwili baadaye yaani Agosti 29, 1999 zilikutana tena na Yanga kurudi kwenye rekodi ya ushindi kwa kuicharaza Simba mabao 3-0.

Mabao ya mechi hiyo ya 63 ya Dabi ya Karikoo ya Ligi Kuu, yaliwekwa kimiani na Bakari Malima ‘Jembe Ulaya’ dk49 na Mohammed Hussein ‘Mmachinga’ (dk71).

BWANA HARUSI NAYE

Agosti 5, 2000 ikiwa ni Dabi ya 65 za Ligi ya Bara, Simba na Yanga zilikutana tena na ‘Bwana Harusi’, Idd Moshi ‘Mnyamwezi’ aliyeacha fungate aliwazima Wekundu wa Msimbazi kwa mabao mawili swafiii na kuwapa vijana wa Jangwani ushindi wa mabao 2-0.

Miaka miwili baadaye timu hizo zilikutana tena katika Dabi ya Agosti, safari hii ikipigwa Jumapili ya Agosti 18, 2002 na mechi kuisha kwa sare ya 1-1, Simba ikitangulia kupata bao kupitia, Madaraka Selemani ‘Mzee wa Kiminyio’ (dk65) kabla ya Sekilojo Chambua kuchomoa bao kwa penalti katika dakika ya 89.

Kisha zikafuata mechi mbili za Ligi ya Bara za wababe hao ambazo zote Simba iliitambia Yanga, ikianza Agosti 7, 2004 ilipoichapa 2-1, mabao yaliyofungwa na Shaaban Kisiga ‘Malone’ (dk 64) akichomoa bao la utangulizi la Yanga lililowekwa kimiani na Pitchou Kongo (dk48), kisha Ulimboka Mwakingwe akamaliza kazi dakika ya 76 kwa kuweka chuma cha pili kuipa Simba ushindi wa pili ndani ya Agosti.

Simba ilinogewa tena kwani Agosti 21, 2005 zilipokutana tena katika Dabi ya Ligi ndani ya mwezi huo, ilishinda mabao 2-0 ikiwa ni ushindi wa tatu kwao mbele ya Yanga kwa Agosti.

Mabao ya ushindi kwa Simba katika mechi hiyo iliyopigwa kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha yaliwekwa kimiani na nahodha Nico Nyagawa dakika za 22 na 56 na kufanya rekodi ya vigogo hao kwa Ligi ya Bara ndani ya Agosti kuwa mechi 11, huku Yanga ikishinda sita, Simba tatu na nyingine mbili zikiisha kwa sare.

NJE YA LIGI SASA

Dabi ya Kariakoo hazikuishia kwenye Ligi ya Bara tu, kwani hata katika mechi za michuano mingine timu hizo zimeshakutana mara sita tofauti, huku Simba ikionekana kutisha kwa kushinda mara nne, dhidi ya mbili za Yanga.

Timu hizo zilianza kukutana katika nusu fainali ya Kombe la Tusker iliyokuja kutumika pia kama mechi za Ngao ya Jamii Agosti 15, 2006 na dakika 90 ziliiisha kwa sare ya bao 1-1 kisha Simba kushinda katika hatua ya penalti ikizamisha mikwaju 7-6.

Katika dakika za kawaida, Simba ilitangulia kupata bao kupitia Emmanuel Gabriel ‘Batigol’ (dk69) kabla ya Credo Mwaipopo kuchomoa (dk90) na kupeleka pambano kwenye penalti na Mnyama kutakataka.

Baada ya hapo mara michuano ya Ngao ya Jamii ilipoanza kuchezwa rasmi nje ya michuano ya Tusker, vigogo hivyo vilikutana tena Agosti 18, 2010 ambapo mechi iliisha kwa suluhu na Yanga kushinda 3-1.

Agosti 17, 2011 timu hizo zikakutana tena katika Ngao ya Jamii ndani ya Agosti na Simba kushinda mabao 2-0 yaliyofungwa na Haruna Moshi ‘Boban’ (dk15) na Felix Sunzu (dk38).

Miaka minane baadaye timu hizo zikakutana tena katika Ngao ya Jamii ndani ya Agosti na Simba kushinda kwa penalti 5-4 baaada ya dakika za kawaida kumalizika kwa suluhu. Mechi hiyo ilipigwa Agosti 23, 2017.

Mwaka juzi timu hizo zilikutana tena katika Ngao ya Agosti, iliyopigwa Kwa Mkapa na Yanga kushinda mabao 2-1. Mechi hiyo ilipigwa Agosti 13, 2022 na Fiston Mayele aliwatungua kwa mara nyingine Simba baada ya msimu mmoja nyuma kuwafunga pia kwa bao 1-0.

Mayele alifunga mabao ya Yanga dakika ya 50 na 81 baada ya Simba kutangulia kwa bao la dakika ya 16 kupitia kwa winga, Pape Ousmane Sakho na mwaka jana katika tarehe kama hiyo ya Agosti 13, Simba ilitwaa Ngao kwa penalti 3-1 baada ya dakika za kawaida kuisha kwa suluhu Mkwakwani, Tanga.

ALHAMISI MMH

Rekodi zinaonyesha, mechi za Dabi ya Kariakoo zimechezwa mara mbili tu siku ya Alhamisi na leo itakuwa ni ya tatu. Yanga imeshinda mchezo mmoja na mwingine uliisha kwa sare.

Zilikutana mara ya kwanza Alhamisi ya Aprili 29, 1982 na bao la dakika ya pili la Rashid Hanzuruni lilitosha kuua Mnyama na zilipokutana tena Alhamisi ya Februari 10, 1983 timu hizo zilishindwa kutambiana kwa kutoka suluhu. Leo nani atacheka?

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: