Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Rekodi 10 ngumu kuvunjwa Ligi ya Mabingwa Ulaya

Messi And Ronaldo UEFA Rekodi 10 ngumu kuvunjwa Ligi ya Mabingwa Ulaya

Sat, 1 Jun 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Rekodi zinawekwa ili zivunjwe. Lakini, si kwa rekodi hizi.Kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, ambapo usiku wa leo Jumamosi itashuhudiwa mechi kali ya fainali baina ya Real Madrid na Borussia Dortmund huko uwanjani Wembley, zitavunjwa rekodi nyingi, lakini kuna ambazo hazitaguswa.

Wakati mashabiki wakisubiri kipute hicho matata kabisa kitakachomshuhudia kiungo Jude Bellingham akikutana na timu yake ya zamani, kuna rekodi zinasubiriwa kuona kama zitaweza kuvunjwa. Lakini hizi rekodi, kuvunjwa ni ngumu.

Bao la haraka

Anayeshikilia rekodi hiyo ni Roy Makaay, kwenye sekunde ya 10.12. Bao hilo lilifungwa 2007 na tangu wakati huo, hadi sasa hakuna bao jingine lililofungwa ndani ya muda huo. Kitu kizuri ni kwamba Mdachi, Roy Makaay alifunga dhidi ya Real Madrid. Los Blancos itaingia uwanjani usiku wa leo, kitu itapaswa kufanya ni kukwepa kuvunja rekodi yao ya kufungwa bao la mapema zaidi kwenye historia ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Mabao mechi moja

Mabao 12 kwenye mechi moja iliyokutanisha Borussia Dortmund na Legia Warsaw mwaka 2016.

Ndio ni mabao 12 na kipute hicho kilifanyika uwanjani Signal Iduna Park. Kipindi hicho, Dortmund ikiwa chini ya kocha Thomas Tuchel haikuwa kwenye kiwango kizuri sana, hivyo kocha huyo Mjerumani alihitaji kuwa na mastaa wake wote uwanjani. Na hakika mambo yalikuwa vizuri, Shinji Kagawa na Marco Reus walikuwa miongoni mwa waliotikisa nyavu, mmoja akifunga mbili na mwingine hat-trick. Si matokeo unayotarajia kuyaona siku za karibuni. Ilikuwa 8-4.

Mashabiki wengi uwanjani

Mechi za Ligi ya Mabingwa Ulaya zimekuwa zikivutia mashabiki wengi kwenda kuzishuhudia viwanjani, lakini kipute cha Barcelona na Paris Saint-Germain katika msimu wa 1994/95 kilikuwa cha kibabe sana, ambapo mashabiki 115,000 walifika uwanjani Nou Camp kushuhudia mchezo huo. Mastaa kama Ronald Koeman na Pep Guardiola walikuwa uwanjani kwenye mechi hiyo. Wawili hao kwenye mafanikio yao wakiwa wachezaji na sasa wakiwa makocha bado wameweka rekodi ya mechi yao kuvutia mashabiki wengi kwenye historia ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Mchezaji mwenye umri mkubwa

Wakati kipa Marco Ballotta aliporuhusu mabao matatu dhidi ya Real Madrid ilikuwa miezi michache sana kabla ya kufikisha umri wa miaka 44, hilo lilimfanya kuvunja rekodi ya Alessandro Costacurta kwa karibu miaka mitatu. Licha ya Gianluigi Buffon alicheza soka akiwa na umri mkubwa, lakini Ballotta anashikilia rekodi ya kuwa mchezaji mwenye umri mkubwa kucheza kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, alipofanya hivyo akiwa na umri wa miaka 43 na siku 253. Mchezaji aliyekuwa akidhaniwa kwamba atavunja rekodi hiyo ni beki wa kati, Pepe, ambaye alicheza akiwa na umri wa miaka 41 na siku 15. Rekodi hiyo bado ipo ipo sana.

Mchezaji mwenye umri mdogo

Mwaka 2020, Youssoufa Moukoko aliweka rekodi ya kuwa mchezaji mwenye umri mdogo kucheza kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, wakati alipofanya hivyo akiwa na umri wa miaka 16 na siku 18. Wiki tatu tangu alipotoka kusherehekea kutimiza umri wa miaka 16, Moukoko aliweka rekodi kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, alipoichezea Borussia Dortmund kwenye ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Zenit St Petersburg. Umri wake ni miaka 19, lakini bado Moukoko hajafanya kitu kikubwa tofauti na matarajio.

Kufunga mechi nyingi mfululizo

Moja ya rekodi itakayodumu kwa muda mrefu kuvunjwa kwe-nye Ligi ya Mabingwa Ulaya ni ile ya kufunga kwenye mechi mfululizo. Rekodi hiyo inashikiliwa na supastaa, Cristiano Ronaldo, aliyeweka rekodi hiyo baada ya kufunga kwenye mechi 11 mfululizo. Ronaldo ameonyesha ubora mkubwa akiweka rekodi hiyo ya kufunga kwenye mechi 11 mfululizo mara mbili tofauti. Ronaldo alianza kwenye fainali ya mwaka 2017, kisha aliendelea kutikisa nyavu kwenye mechi zilizofuatia kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa msimu wa 2017/18, kipindi hicho akiwa Real Madrid.

Kufunga mara nyingi msimu mmoja

Ni supastaa Cristiano Ronaldo tena, aliweka rekodi hiyo ya kibabe kabisa alipofunga mabao 17 kwenye msimu mmoja wa Ligi ya Mabingwa Ulaya. Michuano hiyo ya Mabingwa Ulaya imeshuhudiwa mastraika wengi wenye uwezo mkubwa, lakini hakuna aliyefanikiwa kuvunja rekodi hiyo ya Ronaldo, ambapo kipindi hicho alipokuwa Real Madrid kwenye msimamo huo, alifunga mabao tisa kwenye hatua ya makundi, mabao manne kwenye raundi ya 16 bora, bao moja kwenye robo fainali, mabao mawili kwenye nusu fainali na bao moja kwenye fainali.

Kufunga misimu mingi mfululizo

Supastaa, Lionel Messi wakati huo akikipiga Barcelona, aliweka rekodi ya kufunga mabao kwa misimu 18 kwenye mikikimikiki ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Isingekuwa rahisi kumwona Ronaldo akiweka rekodi zake zisizovunjika kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, kisha ukamkosa mpinzani wake wa miaka yote, Messi. Supastaa huyo wa kimataifa wa Argentina alionyesha kwa namna alivyoweza kutunza ubora wa kiwango chake kwa miaka mingi na hivyo kufanikiwa kufunga mabao kwenye misimu 18 mfululizo kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Mabao mengi kwenye timu moja

Ni supastaa Lionel Messi kwa mara nyingine, akiwa Barcelona aliweka rekodi ya kufunga mabao mengi zaidi kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya akiwa na timu moja. Staa huyo, alifunga mabao 120 kwenye michuano hiyo ya Ulaya akiwa na kikosi hicho cha Nou Camp kabla ya kuondoka kwenda Paris Saint-Germain, ambako pia alihama na kutimkia zake Inter Miami ya Marekani, anakocheza hadi sasa. Rekodi hiyo ya Messi nayo itadumu kwa muda mrefu, kwa sababu itachukua muda kumwona mchezaji mmoja akifunga mabao mengi kwenye klabu moja katika michuano hiyo ya Ulaya.

Kucheza mechi nyingi bila ya kubeba ubingwa

Kipa mkongwe Gianluigi Buffon aliweka rekodi ya kucheza mechi 131 kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, lakini hajabahatika hata mara moja kunyakua ubingwa wa michuano hiyo. Gianluigi Buffon alitamba kwenye timu nyingi, ikiwamo Juventus iliyokuwa kwenye ubora wake na baadaye alikwenda kujiunga na PSG, lakini na huko pia kipa huyo Mtaliano hakubahatika kushinda taji hilo licha ya kucheza mechi 131. Buffon amepoteza fainali kibao.

Chanzo: Mwanaspoti