Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Refa wa Kombe la Dunia kuzihukumu Yanga, Al Hilal

Nabi Refa CAF.png Refa wa Kombe la Dunia kuzihukumu Yanga, Al Hilal

Sat, 1 Oct 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Kocha wa Yanga, Nasreddine Nabi amerejea kazini akitokea Ubelgiji na jamaa amekuwa mbogo akitaka kuona maandalizi ya mchezo ujao wa Ligi ya Mabingwa unakuwa na tija, lakini Shirikisho la Soka Afrika (CAF) limemteua mwamuzi wa Kombe la Dunia kuhukumu mechi ya Yanga dhidi ya Al Hilal ya Sudan.

CAF imeshapanga waamuzi wa mechi zote mbili za timu hizo ukiwamo wa kwanza utakaopigwa Kwa Mkapa Oktoba 8 utakaochezeshwa na Wanyarwanda, huku ile ya marudiano itahukumiwa na refa aliyepo kwenye orodha ya watakaocheza Fainali za Kombe la Dunia 2022 zitakazofanyika Qatar.

Kwa mujibu wa CAF, waamuzi wa mchezo wa kwanza wote wanatokea Rwanda, wakiongozwa na Samwel Owikunda, huku Mutiyimana Diedone na Karangwa Justin watakuwa pembeni na mezani atakuwa ni Hakizimana Louis.

Kwa mchezo wa marudiano utakaopigwa wiki moja baadaye, mwamuzi wa kati atakuwa ni Bamlak Tessema Weyesa ambaye yumo katika orodha ya waamuzi wanane kutoka Afrika waliotajwa kuchezesha michezo ya Fainali za Kombe la Dunia 2022 zitakozofanyika nchini Qatar.

Uteuzi wa Bamlak unaweza kuwa ni nafuu kubwa kwa Yanga kutokana na umakini wa mwamuzi huyo aliyejijengenea heshima kubwa ya kusimama vyema katika kazi yake.

Al Hilal tayari imeshaondoka nchini Sudan na kutua jijini Lubumbashi, DR Congo ikiweka kambi fupi ya maandalizi kabla ya kuja nchini kuanza kupambana na Yanga na ikiwa hapo itacheza kirafiki dhidi ya TP Mazembe.

Chanzo: Mwanaspoti