Mwamuzi aliyepigwa ngumi na rais wa klabu moja ya Ligi Kuu Uturuki ametolewa hospitalini baada ya kukumbabana na majanga hayo.
Soka la Uturuki limeingia dosari kutokana na tukio hilo lilitokea Jumatatu baada ya rais wa klabu ya MKE Ankaragucu, Faruk Koca kumpiga ngumi mwamuzi Halil Umut Meler, baada ya timu yake kuambulia sare ya bao 1-1 dhidi ya Caykur Rizespor.
Picha za Meler zilionyesha uso wake ukiwa umevimba na kuwahishwa hospitalini, lakini sasa ameruhusiwa baada ya kupata nafuu.
Katika tukio hilo, mchezaji Olimpiu Morutan aliifungia Ankaragucu bao katika dakika ya 14 tu ya mchezo, kabla ya Rizespor kusawazisha kwenye dakika za majeruhi kupitia kwa Adolfo Gaich.
Mechi hiyo iliyokuwa na upinzani mkali, ilishuhudiwa wachezaji wawili wakitolewa kwa kadi nyekundu, Ali Sowe wa Ankaragucu na Emirhan Topcu wa Rizespor.
Lakini, balaa likatoke mwisho wa mchezo, ambapo mwamuzi Halil Umut Meler alifuatwa na Faruk Koca, ambaye ni rais wa klabu ya Ankaragucu na kumchapa ngumi kali usoni.
Ngumi hiyo ulimwangusha mwamuzi Meler sakafuni ambako aliendelea kupigwa mateke ya kichwani kabla ya wachezaji na maofisa wengine waliokuwa uwanjani hapo kuingilia kati na kumwokoa mwamuzi huyo.
Muda mfupi, mwamuzi huo alionekana kuwa damu imevilia jichoni na kuhitaji kwenda hospitali kufanyiwa matibabu zaidi.
Koca, 59, ni rais wa Ankaragucu tangu 2021 na mwaka jana alishinda Tuzo ya Uungwana.