Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Refa aitisha Simba Manungu

Manungu Stadium Uwanja wa Manungu Mkoani Morogoro

Sat, 22 Jan 2022 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Straika wa zamani wa Simba, Athumani Machupa amefichua kwamba kwenye mechi yao ya mwisho ndani ya Uwanja wa Manungu, Turiani mwamuzi alianza kuwatisha kwa lugha za kejeli tangu wanaingia Uwanjani ndio maana mechi ikavurugika.

Staa huyo kipenzi cha mashabiki anayesifika kwa kuitesha Yanga kwenye dabi, amekiri kwamba katika mechi hiyo aliingiwa na jazba za ujana na kujikuta akimpiga mwamuzi(ambaye jina lake halipo kwenye kumbukumbu za TFF) kwa madai kuwa hakuwa na maamuzi rafiki kwao.

Kauli hiyo ya Machupa anayeishi Sweden, imekuja siku chache baada ya Bodi ya Ligi kuthibitisha Manungu iko vizuri tayari kwa mechi dhidi ya Simba Jumamosi.

Hiyo ni mara ya kwanza tangu zitokee vurugu za Septemba 11 mwaka 1999, Simba wakiweka mpira kwapani wakiwa wameshachapwa mabao 2-0, msimu huo Mtibwa ikibeba ubingwa.

Dakika ya 78 baada ya Mtibwa Sugar kufunga bao la pili kwa penalti, wachezaji wa Simba hawakukubali na kuanzisha vurugu kwa mwamuzi kabla ya mashabiki wao nao kuingilia kati hivyo kuibuka kwa vurugu kubwa iliyovunja pambano hilo lililofanyika kwenye uwanja wa Manungu Turiani Morogoro.

Baada ya tukio hilo uwanja huo ukafungiwa na tangu hapo Mtibwa haijawahi kucheza na Simba na Yanga kwenye uwanja huo hivyo mechi baina ya timu hizo kufanyika kwenye Uwanja wa Jamhuri Morogoro.

Kumbukumbu hiyo imekuja wakati Mtibwa Sugar ikitangaza kwamba mechi yao ya Jumamosi itafanyika Manungu kwani unakidhi vigezo vyote baada ya kuufanyia ukarabati na kukaguliwa na wataalam wa mamlaka husika.

TUKIO LA 1999

Beki na nahodha wa zamani wa Mtibwa Sugar, Mecky Maxime akitoa ushuhuda alisema mchezo huo ulikuwa mkali na wenye ushindani mkubwa lakini walishangaa Simba kutia mpira kwapani.

“Nakumbuka hadi kipindi cha kwanza kinamalizika tulikuwa tunaongoza bao moja na kipindi cha pili tulirejea kwa nguvu na dakika za mwishoni mwishoni tukapata penalti na tulivyofunga ndipo varangati ilipoanza.

“Wachezaji wa Simba walianza kugomea mchezo wakimzonga mwamuzi, mara vurugu zikaanza hadi mashabiki wakaingi uwanjani na nakumbuka mashabiki wa Simba waliwapaka sana upupu wakazi wa Mtibwa mabao wako jirani na uwanja ,”alisema Maxime.

Naye mchezaji wa zamani wa Simba ambaye alimpiga mwamuzi katika mchezo huo, Athuman Machupa alisema; “Nakumbuka tulikuwa tunaingia uwanjani tu alikuwa anatuambia kwa kejeli kwa sauti ya chinichini kwamba leo hapa hamtoki,” alidai Machupa huku akiwa hakumbuki jina la mwamuzi huyo lakini anajua alitokea Tanga.

“Ilikuwa mwaka 1999, wakati ule kulikuwa na tetesi kwamba TFF (Shirikisho la Soka Tanzania) linataka kuibeba Mtibwa Sugar ili ipate ubingwa.

“Ilitokea vurugu kubwa katika mchezo huo, lakini chanzo ilikuwa ni mwamuzi kuwa upande wa Mtibwa na kutufanyia ndivyo sivyo sisi, ikiwamo kutoa kadi hovyo kwa wachezaji wa Simba,”alidai Machupa.

Alisema yeye wakati ule alikuwa bado mdogo, alimfuata mwamuzi kumuuliza kwanini anaharibu ile mechi lakini akamjibu kwa kejeli.

“Aliniambia wewe dogo, tulia kutokana na umri wangu wakati ule, nilipata hasira nikamchapa kibao, lakini ilikuwa ni ujana tu,” alisema Machupa jana huku akicheka.

Alisema tukio lile lilisababisha baadhi ya wachezaji wa Simba kufungiwa, ingawa yeye alipona kwenye dhahama ya kufungiwa kwavile hakukuwa na ushahidi sahihi wa video.

“Lakini pia sikumpiga peke yangu,mwamuzi alipigwa na watu wengi, nakumbuka mechi ilivunjika tukiwa tumeshafungwa bao 2-0, ndipo vurugu zilianza,” alisema Machupa ambaye kwa sasa anaishi nchini Sweden.

Naye kipa wa Simba aliyekuwa langoni siku hiyo, Mohammed Mwameja, alisema mwamuzi alichangia mechi hiyo kuvunjika kutokana na kuwaonea sana na kuibeba Mtibwa Sugar.

“Chanzo cha vurugu ni mwamuzi kutoa faulo na kutupigia filimbi za kuotea sisi kila wakati sasa jambo hilo tulishindwa kuvumilia na ndio maana tukapandwa na hasira hadi vurugu zikaanza na mchezo kuvunjia “alisema Mwameja

MANUNGU YA SASA

Uongozi wa Mtibwa, umethibitisha kwamba Manungu ya sasa siyo ile ya zamani na kwamba miundombinu yote iko rafiki na salama na hata usalama ndani na nje ya uwanja umeimarika ndio maana wakapewa kibali na mamlaka za juu.

Ofisa Habari za Mtibwa, Thobias Kifaru amesisitiza kwamba wamejipanga kikamilifu na mashabiki na wapinzani wao waje bila wasiwasi.

Bodi ya Ligi, kupitia kwa Mwenyekiti wake, Steven Mnguto imethibitisha jana kwamba imetuma vyombo vya usalama kujiridhisha na hali halisi ya Uwanja huo. Hatahivyo, juzi Bodi hiyo ilitoa taarifa rasmi kwamba mechi itapigwa Manungu lakini baada ya presha za wadau wakatoa tamko kwamba wanasikilizia vyombo vya usalama.

MTIBWA YA ENZI HIZO

Ilikuwa na; Ali Mohammed, Mecky Maxime, Masumbuko Hassan, Geofrey Magoli,Luben Mgaza Kamba Luffo, Abubakary Mkangwa,James Tungaraza, Thomas Masamaki, Said Mhando na Mudy Salim.

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz