Mechi ya ufunguzi wa mashindano ya mataifa ya Afrika (AFCON) 2023 kati ya Ivory Coast na Guinea Bissau kesho jijini Abidjan katika Uwanja wa Olimpiki wa Alassane Ouattara kuanzia saa 5:00 usiku itachezeshwa na refa Mohamed Amin kutoka Misri.
Hii ni mara ya tatu kwa refa huyo mwenye umri wa miaka 38 kuchezesha fainali za AFCON baada ya kufanya hivyo katika fainali za mwaka 2019 na zile za mwaka 2021.
Mwamuzi huyo atasaidiwa na Wamisri wenzake Mahmoud Abou El-Regal, Ahmed Hossam Taha na refa wa akiba Mahmoud Maarouf wakati kwenye teknolojia ya usaidizi wa video kwa waamuzi watakuwepo pia Wamisri, Mahmoud Ashour na Mahmoud El-Banna.
Amin aliyeteuliwa kuchezesha mechi ya ufunguzi anasifika kwa kumwaga kadi kwa wachezaji watovu wa nidhamu na wale wacheza rafu jambo ambalo hapana shaka linawalazimisha nyota wa Ivory Coast na Guinea Bissau kuwa makini katika mechi ya kesho.
Kumbukumbu zinaonyesha katika mechi 10 zilizopita za mashindano tofauti ambazo Amin amechezesha, alitoa idadi ya kadi 45 ambapo kati ya hizo, kadi nyekundu ni tatu na kadi za njano ni 42.
Ikumbukwe kwamba Tanzania haina refa katika fainali za AFCON mwaka huu ingawa itategemea uwakilishi wa marefa 12 kutoka nchi wanachama wa Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) ambao wamepata fursa hiyo.
Marefa 12 ambao wataiwakilisha CECAFA kwenye AFCON mwaka huu ni Peter Waweru, Gilbert Cheriot na Yiembe Stephen kutoka Kenya, Bamlak Tessema (Ethiopia), Mahmoud Mahmood, Ibrahim Mohamed na Mohamed Ibrahim (Sudan), Samuel Uwikunda na Salima Mukasanga (Rwanda), Pacifique Ndabihawenimana (Burundi), Liban Abdoulrazack (Djibouti) na Omar Artan (Somalia).
Fainali za AFCON zinashirikisha timu za taifa 24 ambazop zimegawanywa katika makundi manne yenye timu nne kila moja ambapo timu mbili zitakazoongoza kila kundi zitafuzu hatua ya 16 bora.
Timu hizo 24 ni Ivory Coast, Guinea Bissau, Guinea Ikweta, Nigeria, Misri, Ghana, Cape Verde, Msumbiji, Senegal, Cameroon, Gambia, Guinea, Tunisia, Mali, Afrika Kusini, Namibia, Algeria, Mauritania, Burkina Faso, Angola, Morocco, Tanzania, DR Congo na Zambia.