WINGA wa zamani wa Yanga, Edibily Lunyamila amesema miongoni mwa wachezaji waliomvutia hadi sasa baada ya Ligi Kuu Bara kuchezwa raundi tano ni kiungo mshambuliaji Ramadhan Chombo ‘Redondo’, Denis Nkane wote kutoka Biashara United na Feisal Salum ‘Fei Toto’ wa Yanga.
Sambamba na hao aliwataja pia beki wa Yanga, Yannick Bangala na mshambuliaji wa Polisi Tanzania, Vitalis Mayanga pamoja na beki wa kushoto wa Simba, Mohamed Hussein huku akisisitiza kuwa ni mapema sana kutoa tathmini kwani mzunguko wa kwanza wa ligi utakapomalizika utatoa majibu mazuri.
Nyota huyo wa zamani wa Yanga, Simba, Biashara Shinyanga na Malindi alitoa tathmini hiyo alipozungumza na Mwanaspoti huku akipongeza ushindani uliopo kwenye ligi msimu huu kwa kila timu kutafuta ushindi bila woga ama kujali nyumbani au ugenini.
“Ligi ni ya ushindani na hili linaonekana kwenye matokeo, tazama hadi sasa hakuna timu iliyofungwa mabao zaidi ya matatu. Kwa hiyo ni ligi ambayo timu zote zimejipanga nadhani wadhamini Azam Media wameleta changamoto.
“Vijana wanapambana naamini baada ya mzunguko wa kwanza ndiyo tunaweza kutathmini kama muendelezo utakuwepo manake wengine wanaanza vizuri lakini baadae wanapotea, wachezaji kama Redondo, Mayanga, Feisal Toto, Bangala, Nkane na Tshabalala pia wamejitahidi,” alisema.
Kuhusu hali ya mwenendo wa Simba, alisema: “Siyo Simba tu hata Geita Gold hawajaanza vizuri lakini hatuwezi kusema wameanza vibaya maana ligi inapoanza kila timu inataka matokeo mazuri lakini baada ya raundi ya 10 mambo yanaweza kubadilika kukawa na ushindani,”
Staa chipukizi wa Biashara United, Nkane alitoa ya moyoni akisema: “Lunyamila ni miongoni mwa wachezaji wakubwa na nembo katika soka la nchi yetu, bila shaka kuona nachofanya inanipa hamasa kuongeza juhudi zaidi na kuimarika ili niendelee kuisaidia klabu yangu na baadae timu ya taifa,”