Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Red Arrows yaandika historia Kagame Cup 2024

Kagame Pict Red Arrows

Mon, 22 Jul 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Michuano ya Kombe la Kagame 2024 imefikia tamati jana jioni, kwa timu ya Red Arrows ya Zambia kutwaa ubingwa wa michuano hiyo baada ya kuifunga APR ya Rwanda kwa penalti 10-9 kwenye mchezo wa kuvutia wa fainali uliopigwa kwenye Uwanja wa KMC, jijini Dar es Salaam.

Red Arrows inakuwa timu ya kwanza kutoka nje ya Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati kubeba taji hilo tangu michuano hiyo ilipoasisiwa mwaka 1967, baada ya dakika 120 za pambano hilo la fainali kumalizika kwa sare ya bao 1-1.

Katika dakika 90 za kawaida, timu hizo zilimaliza kwa kufunga mabao hayo, Red Arrows ikianza kutangulia kupitia kwa Ricky Banda aliyetumia mpira kambani dakika ya 63 kabla ya Mamadou Sy kuchomoa bao hilo dakika ya 90 na kufanya mchezo kwenda kwenye muda wa ziada ambao pia zilishindwa kufungana.

Ndipo zikaja penalti ambapo tano za mwanzo kila moja ikikwamisha wavuni na kufuatiwa na piga nikupige hadi penalti ya 10 ambapo APR ilipaisha ile ya mwisho na Red Arrows ikatupia nyavuni na kuipa timu hiyo ya Zambia taji hilo na kitita cha Dola 30,000 (zaidi ya Sh 80 Milioni).

Hii inakuwa ni mara ya kwanza timu ya kwanza ya Zambia kufika fainali za Kagame, lakini pia ya kwanza kutoka nje ya Ukanda wa Cecafa kutwaa taji hilo, kwani mara tatu tofauti timu kutoka Ukanda wa Kusini mwa Afrika (Cosafa) zilishatinga fainali, lakini ziliishia patupu kwa kufungwa.

Timu ya kwanza kucheza fainali ya michuano hiyo ilikuwa ni Rio Tinto ya Zimbabwe mwaka 1982 ilipopoteza mbele ya AFC Leopards ya Kenya, kisha zikafuata timu za Malawi, ADMARC Tigers mwaka 1983 ilipofungwa pia na Leopards kwa mabao 2-1 na Big Bullets ilichezwa mwaka 2021 na kulala 1-0 na kwa Express ya Uganda.

Kipa wa APR Pavel Ndzila alichaguliwa kuwa kipa bora wa michuano hiyo, huku Mohamed Abdelrahmana akiwa Mfungaji Bora kwa mabao matano aliyofunga na mchezaji Bora alikuwa ni Clement Niyigena ambao kila mmoja alivua dola 2,000 (zaidi ya Sh 5 milioni).

Hii ilikuwa ni fainali ya tisa kwa APR ambayo imebeba mataji mara tatu mwaka 2004, 2007 na 2010, huku ikipoteza michezo mingine mitano ya fainali.

Katika mechi ya mshindi wa tatu, Al Hilal ilipata ushindi pia kwa penalti 3-2 dhidi ya Al Wadi baada ya dakika 90 kumalizika kwa sare ya 1-1.

Al Hilal iliyokuwa ikipewa nafasi kubwa ya kubeba kwa mara ya kwanza taji la michuano hiyo, hasa baada ya Simba, Yanga na Azam kuchomoa kushiriki, ilipata nafasi hiyo kwa ushindi wa penalti 3-2 baada ya dakika 120 kumalizika kwa sare ya bao 1-1, huku timu hiyo ikipoteza penalti mapema kipindi cha kwanza.

Pape Abdou alikosa penalti dakika ya 35 baada ya kipa wa Al Wadi kuucheza, lakini dakika nne baadae Altayeb Abakaer aliifungua Al Hilal bao la kuongoza.

Hata hivyo, bao hilo lilidumu kwa dakika tatu tu, kwani nahodha wa Al Wadi, Mohamed Adan alisawazisha na kufanya hadi mapumziko matokeo kuwa 1-1.

Kipindi cha pili licha ya timu zote kufanya mabadiliko na kupambana kusaka mabao mengine, lakini dakika 90 za pambano hilo lililopigwa kuanzia saa 6:00 mchana matokeo yalisalia kama ilivyo na timu hizo kupigiana penalti tofauti na ilivyokuwa katika nusu fainali zilichezwa kwa dakika 120 baada ya kuongezewa muda.

Kinara wa mabao wa michuano hiyo, Mohammed Abdelrahman aliyemaliza akiwa na mabao matano, ndiye aliyeihakikishia Al Hilal inayonolewa na kocha Florent Ibenge kwa kufunga penalti ya ushindi baada ya awali timu hiyo kupoteza mbili na Al Wadi ikapoteza ya mwisho.

Kwa matokeo hayo, Al Hilal imetwaa Dola 10,000 zaidi ya Sh 26 Milioni, fedha zinazotolewa na mdhamini mkuu wa michuano hiyo iliyoasisiwa mwaka 1967, Rais wa Rwanda, Paul Kagome aliyeziweka tangu 2002.

Michuano hiyo ilianza Julai 9 ikishirikisha klabu 12 zilizopangwa makundi matatu, huku wenyeji Singida Black Stars, JKU na Coastal Union zilishindwa kuvuka kwenda nusu fainali.

Vigogo Simba, Yanga na Azam zilizochomoa kushiriki michuano hiyo kutokana na kubanwa na ratiba ya kambi za maandalizi ya msimu mpya wa mashindano kwa mwaka 2024-2025.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live