Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Real Madrid wamnyatia Jurgen Klopp

Jurgen Klopp Real Madrid Jurgen Klopp

Tue, 14 Feb 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Habari nd’o hiyo. Real Madrid inahitaji huduma ya Kocha Jurgen Klopp na mchakato wote wa kumnasa utafanyika mwishoni mwa msimu huu.

Na katika mpango huo wa kumnasa kocha huyo wa Kijerumani anayeinoa Liverpool kwa sasa, utatanguliwa na mkakati kabambe wa kunasa saini ya kiungo Mwingereza, Jude Bellingham anayekipiga huko Borussia Dortmund.

Mabosi wa Santiago Bernabeu wanaamini kwamba usajili wa Bellingham utaweza kumshawishi Klopp akaamua kuachana na Anfield ili akapige kazi kwao.

Klopp, 55, aliongeza mkataba huko Merseyside, Aprili mwaka jana - ambapo alisaini dili la kumfanya abaki kwenye kikosi hicho hadi 2026.

Lakini, kila kitu kinaweza kubadilika baada ya Liverpool kuwa kwenye kiwango kibovu sana msimu huu. Miamba hiyo ya Anfield, usiku wa jana Jumatatu ilitarajia kukipiga na Everton kwenye kipute cha Merseyside derby na kabla ya mechi hiyo ilikuwa ikishika nafasi ya 10 kwenye msimamo wa ligi jambo linalomfanya Klopp kuwa kwenye presha kubwa ya kufikiria hatima ya ajira yake.

Wakati miaka yake saba kwenye kikosi hicho ikiwa na mafanikio makubwa, lakini mwenendo wa Liverpool kwa sasa unatishia maisha ya Klopp kufika ukingoni.

Kwa mujibu wa El Nacional, Klopp akiachana na Liverpool basi, Real Madrid itakwenda haraka kunasa huduma ya bosi huyo wa zamani wa Borussia Dortmund.

Kocha wa sasa wa Los Blancos, Carlo Ancelotti ana mkataba unaomfanya aendelee kubaki Bernabeu hadi mwishoni mwa msimu ujao wa 2023/24.

Lakini, Real Madrid inazidiwa pointi 11 na Barcelona kwenye msimamo wa La Liga, hivyo kama hakutakuwa na taji lolote msimu huu, ukiliweka kando taji la Klabu Bingwa Dunia - jambo hilo litamfanya Ancelotti afunguliwe mlango wa kutokea.

Na Rais wa Los Blancos, Florentino Perez siku zote anavutiwa na Klopp - ambaye amekuwa bora na klabu za Mainz, Dortmund na Liverpool. Na kinachoripotiwa Real Madrid itajaribu kuwasajili Bellingham na Kylian Mbappe ili kumshawishi Klopp kutua Bernabeu.

Bellingham, 19, anathaminishwa na Pauni 100 milioni, amekuwa akihusishwa na klabu kadhaa zinazohitaji huduma yake huko Ulaya.

Real Madrid, Liverpool, Manchester United, Manchester City na Chelsea zote kwa nyakati tofauti zimetajwa kuhitaji huduma ya Mwingereza huyo.

Bellingham anatarajia kuachana na Dortmund kwenye dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi baada ya kudumu kwenye klabu hiyo kwa miaka mitatu - mahali ambako amechagua mabao 44, akifunga 20 na kuasisti 24 katika mechi 117.

Na Klopp ni shabiki mkubwa wa kiungo huyo kinda, ambaye alipandisha thamani yake baada ya kufanya vyema kwenye fainali za Kombe la Dunia 2022 Qatar.

Mbappe, 24, ni mchezaji mwingine ambaye Klopp amekuwa akivutiwa naye. Supastaa huyo Mfaransa hatima ya maisha yake huko Paris Saint-Germain imekuwa kwenye mashaka makubwa baada ya mabingwa hao wa Ligue 1 kuripotoiwa kukubaliana na ishu ya mchezaji huyo kuondoka Oktoba mwaka jana.

Mbappe alisaini mkataba mpya Parc des Princes kwenye dirisha lililopita la majira ya kiangazi ambapo atatakiwa kubaki Paris hadi 2025, lakini bado kuna uwezekano mkubwa wa kuondoka kwenye dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi kama Real Madrid wataweka mezani ofa ya mkwanja wa maana.

Chanzo: Mwanaspoti