Wakati Prisons ikitangaza kuachana na aliyekuwa kocha mkuu wa timu hiyo, Fredi Felix ‘Minziro’ imeandika rekodi kwa kuwa mwiba kwenye mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu kwa misimu mitatu mfululizo.
Prisons ilitangaza mapema jana kufikia makubaliano na Minziro ya kuachana ikiwa ni baada ya kuiongoza michezo tisa na kukusanya pointi saba kufuatia ushindi mchezo mmoja, sare nne na kupoteza nne na kuwa nafasi ya 14.
Minziro alijiunga na timu hiyo yenye makazi yake jijini Mbeya mapema msimu huu ambapo hakuwa na matokeo mazuri na kujikuta akitupwa nje nafasi yake kukaimiwa na msaidizi wake, Shaban Mtupa wakati mabosi wakisaka mbadala wake.
Pamoja na kutemwa kwa Kocha huyo aliyewahi kuzinoa timu kadhaa ikiwamo Geita Gold aliyoipa mafanikio, lakini rekodi zinaonesha kuwa Prisons imekuwa mwiba kwenye mzunguko wa kwanza kwa kubadilisha makocha.
Ikumbukwe msimu wa 2021/22 ilishindwa kumaliza ligi na aliyekuwa kocha wake, Salum Mayanga baada ya kuingia mitini kufuatia matokeo ambayo hayakuwa rafiki na nafasi yake kuzibwa na Patrick Odhiambo raia wa Kenya.
Hata hivyo, Odhiambo naye baada ya kumaliza msimu huo, 2022/23 hakumaliza ligi baada ya kutemwa kutokana na matokeo mabaya nafasi yake kuzibwa na Abdalah Mohamed ‘Baresi’. Minziro naye amekutwa na jinamizi hilo baada ya kuiongoza mechi tisa na sasa ndoa yake na Maafande hao imefikia tamati mapema jana asubuhi na sasa anasakwa mrithi wake atakayeendeleza gurudumu hilo.
Prisons ilifika timu ya saba msimu huu kuachana na kocha wake, ikizifuata Simba iliyomfungia virago Kocha Roberto Oliveira, Zuberi Katwila (Ihefu), Mwinyi Zahera (Coastal Union), Habibu Kondo (Mtibwa Sugar), Cedrick Kaze (Namungo) na Hans Van Pluijm wa Singida Fountain Gate.
Akizungumza na Mwanaspoti, Minziro (pichani) alisema licha ya kusitishiwa mkataba wake lakini ameacha timu katika ari na morali na kwamba ni mapema kujua uelekeo wake akisubiri kulipwa stahiki zake.
Alikiri kuwa imekuwa mshtukizo kwake kupokea uamuzi wa mabosi wa timu kutokana na maandalizi aliyokuwa nayo kwa ajili ya mchezo ujao dhidi ya Coastal Union, utakaopigwa kesho Alhamisi Uwanja wa Sokoine jijini hapa.
“Timu ilikuwa mebadilika ndani ya uwanja na nilikuwa kwenye maandalizi mazuri kwa ajili ya mechi ijayo, ila kwa ujumla vijana nimewaacha kwenye ari na morali, kujua wapi naelekea ni mapema nasubiri wakamilishe stahiki zangu,” alisema Minziro.