Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Raundi 6 ngumu kwa makocha Ligi Kuu

Azam Mateso.png Raundi 6 ngumu kwa makocha Ligi Kuu

Mon, 30 Oct 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Usemi wa ‘kocha huajiriwa ili atimuliwe’ umekuwa ukitumika nchini pindi ajira ya kocha inapofikia tamati iwe kwa kufukuzwa kazi au kuvunja mkataba kwa makubaliano binafsi.

Maana ya usemi huu inaweza kulenga kuonyesha kuwa hakuna kocha anayeweza kudumu kwenye timu miaka yote, lakini kwa hapa nyumbani imekuwa ikitumika tofauti na kama uhalalisha tabia ya timuatimua ya makocha ambayo imekuwa ikifanywa na timu.

Sababu nyingi zimekuwa zikichangiamakocha wengi kupoteza ajira huku kubwa ikiwa ni ile ya matokeo yasiyoridhisha kwa timu ambayo ndio imekuwa haina utetezi iwapo inatumika katika kusitisha kibarua cha kocha.

Ukiondoa hiyo, sababu nyingine inaweza kuwa ni uhusiano usioridhisha baina ya kocha na ama wachezaji au wasaidizi wake katika benchi la ufundi au hata viongozi, lakini pia suala la maslahi binafsi nalo linaweza kusababisha safari ya kocha ndani ya timu fulani ifike kikomo.

Hata hivyo, ingawa suala la kocha kuachana na timu ama kwa kutimuliwa au kuvunja mkataba kwa makubaliano binafsi ni la kawaida, sio jambo linalopendeza kuona idadi kubwa ya makocha wanaonyeshwa mlango wa kutokea mapema katika msimu.

Japo sio jambo jema, tayari imelishuhudiwa katika msimu huu ambao maisha ya makocha yameonekana kuanza kuwa magumu mapema tu ambapo katika raundi sita tu za mwanzo, tayari i makocha watano wameshaachana na timu zao zinazoshiriki Ligi Kuu Bara na wapo wengine zimewaweka katika nafasi finyu ya kubakia katika vibarua ya kuendelea kuvinoa kwa muda mrefu vikosi vyao.

Spoti Mikiki inakuletea orodha ya makocha watano ambao ndani ya muda mfupi wameshaachana na timu kwa sababu tofauti na wengine ambao wamekalia kuti kavu.

Hans Pluijm

Katika msimu uliopita, mambo yalionekana kumnyookea vyema kocha Hans Pluijm ndani ya kikosi cha Singida Big Stars ambacho alikiwezesha kufanya vyema katika Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC).

Pluijm hakuonekana katika uwezekano wa kutimuliwa baada ya kuiongoza timu hiyo kumaliza katika nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi huku kwenye ASFC akiiongoza kufika hadi katika hatua ya nusu fainali.

Lakini mambo yalionekana kugeuka kwake katika msimu huu kutokana na timu hiyo kuanza kwa mwendo usioridhisha ikishindwa kutamba katika mashindano ya Ngao ya Jamii ambapo ilishika nafasi ya nne baada ya kufungwa mechi zote mbili huku ikishindwa kupata ushindi katika mchezo wa kwanza wa ligi dhidi ya Tanzania Prisons ambao ulimalizika kwa sare tasa na pia kupoteza mechi ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya JKU kwa mabao 2-0.

Hilo lilichangiakocha huyo

kuamua kujiweka kando ingawa habari kutoka ndani ya timu hiyo zilifichua kuwa alitimuliwa kimyakimya.

“Kocha wetu Hans van der Pluijm hatutaendelea nae. Timu yetu itakuwa chini ya kocha msaidizi, Mathias Lule mpaka pale itakapoamuliwa vinginevyo,” ilifafanua taarifa ya Singida Big Stars kuachana na Pluijm.

Ernst Middendorp

Baada ya kuongozwa kwa muda na Mathias Lule, Singida Big Stars iliamua kumpa mikoba ya kudumu kocha raia wa Ujerumani, Ernst Middendorp kwa mkataba wa mwaka mmoja.

Kibarua cha kwanza cha kocha Middendorp katika kikosi cha Singida Big Stars kilikuwa ni dhidi ya Future FC ya Misri katika raundi ya kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika ambapo timu hiyo ingefanya vizuri katika mechi mbili baina yao ingetinga katika hatua ya makundi.

Mambo yalianza vyema kwa Middendorp baada ya kuiongoza Singida Big Stars kuibuka na ushindi wa bao 1-0 nyumbani dhidi ya timu hiyo ya Misri lakini siku chache baadaye aliondoka ghafla na kutangaza kuachana na timu hiyo kwa kile alichodai kuwa anaingiliwa na uongozi katika majukumu yake.

“Mamlaka za Singida Fountain Gate zilipanga kikao cha haraka siku iliyofuata kikihusisha timu nzima ya ufundi pasipo kuelezea sababu za kikao. Tulitegemea kutakuwa na neno la pongezi lakini hiyo haikuwa jambo lenyewe. Lengo la kikao lilikuwa wazi kuwa kuelezea kutoridhishwa, maoni yangu hayakusikilizwa na majadiliano hayakuzaa matunda,” alifafanua Middendorp katika sehemu ya barua yake ya kujiuzulu.

Zuberi Katwila

Ihefu ilianza na mwendo wa wastani katika Ligi Kuu msimu huu ambapo katika mechi tatu za mwanzo ilipata ushindi mara moja na kupoteza michezo miwili.

Ushindi katika mchezo wa nne dhidi ya Yanga ulionekana kama ungeweka salama kibarua cha kocha Zuberi Katwila lakini ikaja kupoteza mchezo uliofuata dhidi ya KMC.

Kupoteza dhidi ya KMC kunaripotiwa kulianza kuweka rehani kibarua cha Katwila na siku tatu baadaye kulitolewa taarifa ya mkataba wa Ihefu na Kocha huyo kufikia tamati kwa makubaliano binafsi.

Hata hivyo, Jumatatu wiki hii, Katwila alitangazwa rasmi kama kocha mkuu mpya wa Mtibwa Sugar.

Habibu Kondo

Msimu umeonekana kutoanza vizuri kwa Mtibwa Sugar ambapo katika mechi sita za mwanzo za Ligi dhidi ya Simba, Dodoma Jiji, Coastal Union, Singida Big Stars, Tanzania Prisons na Kagera Sugar haikupata ushindi na ikipoteza michezo minne.

Pamoja na kuonyesha kiwango bora katika mchezo wa kwanza dhidi ya Simba ambao ilipoteza kwa mabao 4-2, Mtibwa Sugar mambo yalionekana kuiendea kombo hasa katika safu yake ya ulinzi ambayo imekuwa ikiruhusu mabao mara kwa mara.

Hilo lilitosha kuushawishi uongozi wa Mtibwa Sugar kuamua kumfungulia milango kocha huyo ambaye nafasi yake imezibwa na Katwila.

Cedrick Kaze

Umekuwa ni mwanzo mbaya kwa Namungo FC katika Ligi Kuu Tanzania Bara tangu timu hiyo ilipopanda daraja ambapo imecheza mechi sita zote za mwanzo bila kupata ushindi.

Kocha aliyetegemewa kwamba angeifanya timu hiyo kuwa tishio, Cedrick Kaze ambaye Namungo ilimuajiri baada ya kuachana na Yanga, alionekana kushindwa kuinusuru timu hiyo na mwenendo huo usioridhisha jambo ambalo lilianza kuweka rehani ajira yake.

Baada ya kupoteza mchezo wa raundi ya sita dhidi ya Singida Big Stars nyumbani kwa mabao 3-1, Kaze aliamua kuchukua uamuzi mgumu wa kujiuzulu kuinoa timu hiyo.

WALIOKALIA KUTI KAVU

Mwinyi Zahera

Baada ya msimu uliopita, Coastal Union iliamua kumuajiri kocha Mwinyi Zahera kuwa kocha mkuu wao katika msimu huu.

Hata hivyo katika mechi tano za mwanzo, timu hiyo ilikusanya pointi mbili tu, huku ikipoteza michezo mitatu, jambo lililoanza kumuweka Zahera katika mazingira magumu klabuni hapo.

Dalili za Zahera kutimuliwa na timu hiyo zimeanza kuonekana wazi baada ya Coastal Union kumzuia asisafiri na timu kwenda Mbeya ambako ilikuwa na mchezo uliopita dhidi ya Ihefu SC ambao ulimalizika kwa sare tasa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: