Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ratiba ya Yanga nchini Algeria iko hivi

Taibi Lagrouni Yangaaaaa Ratiba ya Yanga nchini Algeria iko hivi

Wed, 22 Nov 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Meneja wa Kikosi cha Yanga SC, Walter Harrison, amezungumzia hali ya timu baada ya kundi la kwanza kufika nchini Algeria jana Jumanne.

Kundi la kwanza lililokuwa na wachezaji 13, benchi la ufundi na viongozi, liliondoka Dar es Salaam jana alfajiri, kupitia Uturuki, kisha kufika Algeria jioni, huku kundi la pili likitarajiwa kuungana na wenzao leo Jumatano.

Yanga ipo Algeria kwa ajili ya mchezo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika Kundi D dhidi ya CR Belouizdad utakaochezwa Ijumaa ya wiki hii, kwenye Uwanja wa Julai 5.

Akizungumzia hali ya kikosi, Harrison alisema, wanamshukuru Mungu kila kitu kinaenda sawa, huku akitoa ratiba nzima ya mazoezi kabla ya kufika siku ya mechi.

“Tunamshukuru Mungu tumefika salama Algeria, baada ya kundi la kwanza kutoka Dar jana alfajiri na kufika jioni tukipitia Uturuki. Baada ya kufika, timu ilipata mapumziko kidogo kwa ajili ya kupumzisha miili baada ya safari ndefu, kisha tukafanya mazoezi mepesi kwenye gym.

“Tunategemea kundi la pili ambalo ni la wachezaji waliokuwa kwenye timu za taifa ya Tanzania, Uganda, Burkina Faso na Mali watafika leo na hatimaye kuwa kundi zima hapa kwa ajili ya kujiandaa kuelekea kwenye mchezo wetu wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa dhidi ya CR Belouizdad.

“Baada ya timu nzima kuenea siku ya leo, tutafanya mazoezi ya pamoja jioni majira ya saa 1 kwa saa za huku Algeria, ambapo kwa majira ya Tanzania itakuwa saa 3 usiku.

“Kesho pia tutafanya mazoezi ya mwisho kwenye uwanja ambao tutacheza mchezo wetu siku ya Ijumaa, baada ya hapo, timu itarejea kwa ajili ya mapumziko kuweza kusubiri sasa siku ya mchezo ambayo ni keshokutwa.

“Hali ndiyo iko hivyo ya kikosi chetu mpaka sasa hivi, tunamshukuru Mungu kwa hilo, tuna imani wale wanaokuja kujiunga na sisi tutakuwa kundi zima na mwisho wa siku kuweza kuwa pamoja kwenda kuhakikisha tunatimiza malengo yaliyotuleta hapa nchini Algeria ambayo ni kuondoka na pointi tatu kwenye mchezo wetu wa kwanza wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa barani Afrika,” alisema Harrison.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: