Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ratiba Ligi Kuu pasua kichwa

95248 Pic+ligi+kuu Ratiba Ligi Kuu pasua kichwa

Tue, 11 Feb 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wakati mtendaji mkuu mpya wa Bodi ya Ligi, Almas Kasongo akiitaja ratiba kuwa moja ya mambo aliyopanga kuyashughulikia haraka katika Ligi Kuu Bara, muingiliano wa ratiba umeibua mjadala licha ya mwenyekiti wa Bodi, Steven Mnguto kujitetea.

Mjadala umeibuka baada ya mechi ya Azam na KMC na ile ya Yanga na Ruvu Shooting kupangwa kuchezwa muda mmoja kwenye viwanja viwili tofauti vilivyo eneo moja, Dar es Salaam.

Yanga na Ruvu Shooting walicheza Uwanja wa Taifa wakati Azam na KMC wakichezea Uwanja wa Uhuru, viwanja vyote vikiwa vimepakana.

Mbali na mechi hiyo, wachezaji wa Alliance FC walilazimika kuunganisha uwanjani kucheza na Mbao FC, Jumamosi jijini Mwanza, baada ya kusafiri kwa siku tatu mfululizo wakitokea Ruangwa, Lindi, walikocheza na Namungo FC Jumatano iliyopita. Mbao pia ilisafiri kwa zaidi ya saa 48 ikitokea Mtwara ambako walicheza na Ndanda FC.

Kocha wa Alliance FC, Fred Minziro alisema: “Tumeingia Mwanza alfajiri ya kuamkia siku ya mechi Jumamosi, tukafanya mazoezi asubuhi na jioni tukaingia uwanjani, tulicheza ilimradi na Jumanne tuna mechi na Kagera Sugar, Uwanja wa Kaitaba.”

Kocha wa Mbao, Abdulmutik Haji alisema waliomba mechi yao dhidi ya Alliance FC isogezwe mbele, lakini walikataliwa.

Pia Soma

Advertisement
Akizungumzia mvurugano wa ratiba, Mnguto alisema hata wao unawatesa lakini hawana namna. “Mfano mechi za Yanga na Ruvu na ile ya KMC na Azam, moja ilikuwa ichezwe saa 10 na nyingine saa 1 usiku, baadaye tukaambiwa uwanja una tatizo la taa, na Uwanja wa Uhuru umetumika sana unahitaji kupumzishwa. Baada ya majadiliano marefu hatukuwa na namna ikatulazimu mechi zote zichezwe muda mmoja katika eneo moja lakini viwanja viwili tofauti,” alisema.

Kuhusu Alliance FC kusafiri na kisha kuunganisha kwenye mechi, Mnguto alisema hawana jinsi na kwamba wakisema wasogeze mechi mbele ligi itakwenda hadi Juni kinyume na ratiba ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (Caf).

Chanzo: mwananchi.co.tz