Mashabiki wa Manchester United wamevurugwa baada ya kugundua kuwa asilimia 25 za mwekezaji mpya mtarajiwa wa timu hiyo, Sir Jim Ratcliffe hazitawanufaisha katika ishu za usajili.
Mashabiki wamejawa hofu juu ya mustakabali wa klabu yao endapo Ratcliffe atafanikiwa kuchukua asilimia 25 za umiliki.
Kujiondoa kwa Sheikh Jassim licha ya kuweka mezani ofa ya Pauni bilioni 5 mezaji kwa ajili ya kuinunua klabu hiyo kumefungua njia kwa bilionea kutoka Uingereza, Sir Ratcliffe ambaye atasimamia masuala ya michezo.
Mashabiki wa Manchester United
Hiyo inamaanisha kwamba itawaacha wamiliki wa sasa Glazers kuwa wasimamizi wakuu wa klabu hiyo hatua ambayo imepingwa vikali na mashabiki wa Man United wanaoipenda klabu yao.
Mashabiki wamekasirishwa zaidi na madai kwamba endapo Ratcliffe atafanikiwa kununua hisa za Man United haitaongeza uwezo wa matumizi ya aina yoyote katika klabu.
Sheikh Jassim
Kwa mujibu wa gazeti la Guardian, mfanyabiashara huyo anayemiliki kampuni ya Ineos hatabadilisha chochote hususan katika matumizi ya usajili wa wachezaji.
Hizi ni habari mbaya kwa mashabiki wa Man United ambao wamekuja juu kupitia mitandao ya kijamii, na shabiki mojawapo alisema: “Tunajua hilo! Pesa zitaingia kwenye mifuko ya Glazers.”
Mwingine aliandika: “Ni wazi, kwa sababu pesa zote zitaingia kwenye mifuko ya Glazers na wanahisa ambao hawajawahi kuweka hata senti kwenye klabu. Pia tangu siku ya kwanza iliwekwa wazi kuwa hatalipa deni.”
Shabiki wa tatu akaandika: “Hii klabu ndio basi tena” wakati shabiki wa nne alisisitiza: “Hakuna kitakachobadilika, asilimia 25 ya hisa haiwezi kudhibiti masuala makuu ya klabu.”
Man United ilitumia Pauni 180 milioni katika usajili wa dirisha la kiangazi kwa kununua wachezaji wenye majina makubwa kama Rasmus Hojlund, Mason Mount na Andre Onana.
Lakini Mashetani Wekundu bado hawajajipata Ligi Kuu England na Ligi ya Mabingwa Ulaya kwani tayari wamefungwa mechi nne katika mechi nane za ligi.