Tajiri wa Manchester United, Sir Jim Ratcliffe ambaye ndiye anayesimamia shughuli za soka za klabu hiyo, amesema tatizo la timu hiyo kutokufanya vizuri sio Kocha Erik ten Hag.
Mholanzi huyo (53) ataendelea kuwepo msimu ujao baada ya Man united kuamua hivyo, licha ya tetesi nyingi za kusakwa kwa mrithi wake kutokana na matokeo mabovu ya miamba hiyo ya Old Trafford, akiwamo Kocha Thomas Tuchel aliyepigiwa chapuo kutua klabuni hapo.
Pia ilielezwa Man United ingeachana na kocha huyo ambaye alibakiza mwaka mmoja kwenye mkataba wake kama asingebeba Kombe la FA, lakini Ratcliffe akizungumza na tovuti ya Bloomberg, alisema;
"Kocha sio kiini cha tatizo ndani ya Manchester United, hii ni timu ya michezo inatakiwa kuwa na ushindani na ufanisi wa hali ya juu, lakini ili ufanikishe yote hayo inahitajika sapoti, kwa sababu wanaocheza ni wachezaji ambao ndani yao kuna ujana."
Ten Hag alibainisha maeneo yenye changamoto kwenye kikosi chake na kutaka yafanyiwe marekebisho, hata hivyo, amepewa muda wa kukijenga ili kukirudisha kwenye ushindani baada ya misimu miwili au mitatu.
"Sina uhakika sana kama tunaweza kumaliza matatizo yote katika timu kwa dirisha hili la kwanza, kuna matatizo mengi ya kuyashughulikia, nafikiria itachukua madirisha mawili hadi matatu ili kuwa katika nafasi nzuri," alisema Ratcliffe.
Ni miezi sita sasa imepita tangu Ratcliffe aingie kwenye klabu hiyo na kupania kuifanya kuwa tishio tena England na Ulaya huku akiweka wazi mazingira aliyoyakuta ni vigumu timu kuwa na ushindani na aliikuta ikiendeshwa kibiashara zaidi badala ya kimichezo chini ya utawala wa familia ya Glazer.
"Tulikuwa na watu wengi wa hesabu na biashara kuliko wale wa michezo, lakini bado kuna nafasi ya kubadilisha haya katika kila maeneo na sisi tutafanya hivyo, lengo letu ni kufika levo ambazo Real Madrid ipo kwa sasa ingawa hiyo itachukua muda kutimia."