Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Rasmus Hojlund, Leny Yoro hali tete Man United

Hatdgqudyewq Rasmus Hojlund, Leny Yoro hali tete Man United

Tue, 30 Jul 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Baada ya msimu uliopita mastaa wao wengi muhimu kusumbuliwa na majeraha, hofu imetanda tena kuelekea msimu ujao baada ya Rasmus Hojlund na Leny Yoro wote kukumbwa na majeraha katika mchezo wa kirafiki huko Marekani dhidi ya Arsenal wikiendi iliyopita.

Katika mchezo huo Arsenal ilishinda kwa mabao 2-1 na katika kuwapa burudani mashabiki zikapigwa penalti na Mashetani Wekundu wakashinda kwa penalti 4-3.

Hojlund aliitanguliza Man United kwa bao la dakika ya 10 lakini alianguka chini dakika tano baadaye kwa kile kilichoelezwa kwamba alipata majeraha ya nyama za nyuma ya paja.

Arsenal ilisawazisha katika dakika ya 26 kupitia Gabriel Jesus kabla ya Gabriel Martinelli kuweka chuma cha ushindi katika dakika ya 81.

Baada ya mchezo kumalizika waandishi wa habari walimuuliza anajisikiaje, akasema: “Ngoja tuone.”

Mbali ya Hojlund ambaye alikosa pia mechi nyingi za msimu kutokana na majeraha ya mgongo, mchezaji mwingine aliyeumia katika mechi hiyo ni beki Yoro ambaye alikuwa anacheza mechi yake ya pili tangu ajiunge na United akitokea Lille kwa ada ya Pauni 59 milioni katika dirisha hili, naye aliumia dakika ya 33 ya kipindi cha pili.

Kocha Erik ten Hag alipoulizwa kuhusu hali za wachezaji hao wawili baada ya mchezo huo kumalizika alisema: “Ni mapema sana kuanza kuzungumzia hali zao, inatakiwa tusubiri walau baada ya saa 24 ndio tutajua zaidi, tulikuwa na uangalifu mkubwa hususani kwa Leny ambaye amefanya mazoezi kwa asilimia 50 kutokana na kuchelewa kujiunga na timu lakini acha tuone na tuwe na fikra nzuri, juu ya majibu ya vipimo zaidi.”

Moja kati ya mambo ambayo yaliikwamisha sana Man United kwa msimu uliopita ilikuwa ni idadi kubwa ya mastaa wake wa kikosi cha kwanza kupata majeraha ya mara kwa mara.

Katika dirisha hili tayari imeshawasajili wachezaji ambao ni beki wa kati Yoro sambamba na straika wa Bologna, Joshua Zirkzee aliyetua kwa Pauni 36.6 milioni ikiwa ni katika mpango wa kuongeza wingi wa wachezaji na kuhakikisha mmoja akiumia kunakuwa na mwingine mwenye ubora unaofanana.

Akilizungumzia hilo siku chache zilizopita, Ten Hag alisema: “Nahitaji kuwa na kikosi kikubwa kadri inavyowezekana, tayari tumefanya usajili wa wachezaji wawili wazuri sana, kwa hivyo kila mtu anapokuwa fiti tunakuwa na timu ambayo inaweza kushinda mechi yoyote, lakini jambo kubwa zaidi ni kuwa na kikosi kipana, tunatakiwa kuwa na wachezaji wengi kwa sababu tuna mashindano magumu mbele yetu hivyo inabidi tuwe na kikosi kitachokuwa na uwezo wa kucheza hata pale kinapokuwa na majeruhi.”

Mbali ya usajili wa wachezaji, Man United pia iliwaajiri madaktari wawili wapya Gary O’Driscoll na Jordan Reece kutoka Arsenal.

Man United ambayo imepoteza mchezo wake wa pili katika kipindi hiki cha maandalizi ya msimu, baada ya kipigo hicho kutoka kwa Arsenal, itakuwa na mechi dhidi ya Real Betis Agosti 1 kabla ya kuvaana na Liverpool Agosti 4.

Akizungumzia kiwango cha timu yake Ten Hag alisema: “Nafikiri ilikuwa ni mechi nzuri sana kuicheza katika wiki hii ya tatu ya maandalizi ya msimu.”

Chanzo: Mwanaspoti