Serikali imedhamiria kuboresha miundombinu ya michezo hasa katika viwanja ikiwa ni pamoja na kufunga mashine za kisasa za kufuatilia mchezo (VAR) ili kuondoa malalamiko katika michezo na kuandaa timu bora za taifa ambazo zitapeperusha vyema bendera ya nchi katika mashindano ya kimataifa.
Kauli hiyo ilitolewa na Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mohamed Mchengerwa Dar es Salaam juzi wakati wa kikao na viongozi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na Bodi ya Ligi (TPBLP) kujadili mustakabali wa maendeleo ya soka na malalamiko juu ya maamuzi yasiyoridhisha ya waamuzi.
“Tunajipanga kuwa na vyombo vya ufuatiliaji wakati mchezo ukiendelea, tutaanza na viwanja vitano ukiwa ni mpango wa serikali ambao tumeufikiria kwa sababu tunakwenda kufanya maboresho ya miundombinu kwenye viwanja vyetu.”
“Pia ili tuweze kuandaa vizuri timu zetu za taifa hapo mbele, mpango wetu ni uboreshaji wa shule za michezo 56 ambazo zimeibuliwa na dhamira yetu ni kila mkoa kuhakikisha tunakuwa na shule ambazo zitasaidia kuibua vipaji.”
“Sambamba na hilo tunategemea kujenga vituo vitatu vya michezo katika Mkoa wa Dar es Salaam na mikoa mingine ambayo wizara itafanyia kazi,” alisema Mchengerwa.
Pia ameitaka Kamati ya Waamuzi wa mpira wa miguu kijitafakari na kuchukua hatua zaidi dhidi ya waamuzi ambao wameshindwa kutafsiri sheria za mpira wa miguu au kuonesha viashiria vya rushwa, huku akiiagiza TFF kuendesha semina kwa waamuzi kwa kushirikiana na wataalamu kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).
“Pengine TFF wana kazi kubwa ya kufanya, mpaka sasa wamewaondoa waamuzi 13, mpaka ligi inakwisha tunajiuliza watakuwa wamewaondoa waamuzi wangapi? Hivyo ni vyema Kamati ya Waamuzi ikajitafakari ila tunaiachia TFF kwa sababu wao ndio wenye mamlaka,” alisema