Kocha aliyeipa mafanikio makubwa Klabu ya Yanga, Nasreddine Nabi na benchi lake ambalo amekuwa akiambatana nalo, wametia saini ya mkataba wa miaka miwili huku kukiwa na kipengele cha kuongeza mwaka mwingine mmoja zaidi.
Taarifa kutoka nchini Afrika Kusini zimethibitishwa kuwa Nabi sasa ndiye rasmi kocha mkuu mpya wa Klabu ya Kaizer Chiefs ya nchini humo ambayo imekuwa ikinyatia saini ya Mtunisia huyo tangu akiwa Yanga.
Mechi ya keshokutwa Jumapili ya nusu fainali ya Throne Cup ndiyo itakuwa mchezo wake wa mwisho akiwa kama bosi wa FAR Rabat ya Morocco ambako ameshindwa kutwaa Ubingwa wa Ligi ya nchi hiyo licha ya kuongoza kwenye msimamo tangu mwanzo wa msimu lakini mechi za mwisho ndizo zimemharibia na Ubingwa ukabebwa na Raja Casablanca.
Kocha kutoka Ufaransa, Fernando Da Cruz (55) atasafiri kwa ndege kuelekea Afrika Kusini kesho kutayarisha mazingira na kukutana na timu kabla ya kuwasili kwa Nabi ambaye atafanya naye kazi.
"Ndiyo. Pendekezo hilo lilikuwa la kuvutia. Kwa mbinu, tunaweza kubadilisha mambo mengi ili kusaidia timu kurejea kwenye ubora tena,” viongozi wa kaizer wamesema.
Kinachosubiriwa kwa sasa ni kocha huyo kumalizia mchezo wake wa mwisho na FAR Rabat kisha atatangazwa rasmi na AmaKhosi.