Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Rasmi Fei Toto mfalme mpya Chamazi

Feisal Salum Fei Toto Msamah Kiungo wa Azam FC, Feisal Salum "Fei Toto"

Sun, 26 May 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Uongozi wa Azam FC umetamka wazi kiungo mshambuliaji wa timu hiyo, Feisal Salum ‘Fei Toto’ kuanzia sasa ndiye Mfalme wa Chamazi kutokana na ubora aliouonyesha msimu huu.

Fei Toto aliyejiunga na Azam akitokea Yanga, amefunga mabao 18 katika Ligi Kuu Bara akiwa kileleni sawa na Stephane Aziz Ki wa Yanga, huku nyota wote hao wakiwa sio washambuliaji.

Kutokana na kitendo hicho cha kufunga mabao mengi msimu huu, Fei Toto amepewa ufalme huo ambao hapo awali waliwahi kupewa nyota wengine kadhaa kikosini hapo akiwemo Kipre Tchetche.

Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano cha Azam FC, Thabit Zakaria ‘Zaka Zakazi’ amesema ndani ya klabu yao wamepita wachezaji wengi hasa eneo la ushambuliaji lakini wameshindwa kufanya alichofanya Fei Toto, hivyo kiungo huyo anastahili kuwa Mfalme wa Chamazi kuanzia leo.

Zaka Zakazi amebainisha kwamba, Fei Toto alichobakisha ni kuifikia na kuivunja rekodi ya John Bocco aliyoiweka msimu wa 2011-2012 ya kuwa mchezaji wa Azam aliyefunga mabao mengi zaidi (19) katika msimu mmoja wa ligi ambayo imedumu kikosini hapo kwa takribani miaka 12 sasa.

“Nimefurahi kuona Feisal amefunga leo na kufikisha mabao 18 kwa sababu kwenye mpira wanasema ili muendelee kufurahia basi rekodi zivunjwe. Sisi mchezaji aliyefunga mabao mengi kwenye msimu mmoja wa ligi alifunga 19 miaka 12 iliyopita," amesema Zakazi na kuongeza;

“Yaani rekodi hiyo imeshindwa kuvunjwa kwa zaidi ya miaka 10 huku tukiwa tumesajili watu wengi hapa katikati. Kama mna wachezaji hawawezi kuvunja rekodi basi majibu yake wanakuwa wanarukaruka tu. Kama Feisal ataifikia rekodi hii basi ni wazi tutakuwa tunajivunia tumefanya usajili mzuri na umelipa."

Idadi ya mabao aliyonayo Fei Toto kwa sasa imefikia iliyowahi kuwekwa na Mrisho Ngassa akiwa na kikosi hicho cha Azam iliyomsajili pia kutoka Yanga na msimu wa 2010-2011 alifunga 18 na kuwa Mfungaji Bora wa Ligi Kuu kabla ya Bocco kuivunja msimu uliofuata akiwafunga mabao hayo 19.

“Kipre Tchetche mwaka 2013 alifunga mabao 17, alishindwa kuifikia rekodi ya mabao 19, lakini tulifurahia na kumuita king (mfalme) kwa sababu alifunga mabao mengi wakati yeye siyo straika, alikuwa winga. John Bocco alifunga mabao mengi kwa sababu alikuwa straika.

“Straika anatakiwa kufunga mabao mengi kwa sababu ndiyo kazi yake kufunga, kwa hiyo alipotokea winga amefunga mabao mengi tukaona ni kitu cha tofauti, tukamwita king huku tukianza kumtafuta king mwingine.

“Kuna watu wamekuja tumewaita wafalme, sijui mwana wa mfalme lakini wameshindwa, sasa amekuja king mwingine. “Fei sasa anakwenda kuwa King wa Azam Complex hapa Chamazi. Rasmi yeye ndiye King wa Chamazi. Yeye siyo straika bali ni kiungo wa ushambuliaji lakini amefunga mabao 18, tumefurahi sana,” alisema Zaka Zakazi.

Miongoni mwa washambuliaji waliopita Azam na kushindwa kuifikia rekodi ya kufunga mabao 19 ni Idris Mbombo na Prince Dube wakati hivi sasa wapo Alassane Diao na Franklin Navaro ambao wanauguza majeraha.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: