Nyota wa Manchester United, Marcus Rashford, jina lake lilianza kufahamika mwaka 2016, lakini sasa amekuwa mchezaji mwenye jina kubwa akiwa na umri wa miaka 25. Rashford alikuwa hatari msimu uliopita na amemaliza msimu akiwa na mabao 30 ambayo alifunga katika mashindano yote aliyocheza.
Fowadi huyo wa kimataifa wa England alikuwa na mchango katika kikosi cha Erik ten Hag na ameisaidia Man United kubeba taji la Carabao msimu uliomalizika huku wakilikosa Kombe la FA kwa kufungwa na mahasimu wao Man City kwenye mechi ya fainali.
Maisha binafsi
Fowadi huyu alizaliwa Oktoba 31, 1997. Wazazi wake ni Robert Rashford na Melanie Maynard. Alikulia katika jiji la Greater Manchester. Mama yake mzazi alimlea katika mitaa ya Wythenshawe. Vilevile ana dada wawili, Claire na Chantelle na kaka zake wawili Dane Rashford na Dwaine Maynard.
Rashford aliishi na dada na mama yake ambaye aliachana na baba yake. Mama yake alikuwa anafanya kazi katika kampuni ya uhasibu lakini mshahara wake ulikuwa mdogo na haukukidhi mahitaji ya familia.
Malavidavi
Rashford ameachana na mchumba wake Lucia Loi na kushangaza watu wake wa karibu. Staa huyo alimvalisha pete ya mchumba mwaka jana lakini taarifa zimeripoti wawili hao wameachana miezi miwili iliyopita. Rashford licha ya kumiliki utajiri wa pesa ndefu, maisha yake ya uhusiano yamekuwa yakimchanganya sana.
Wawili hao walirudiana mwaka 2021 baada ya kuachana, lakini sasa uhusiano wao umevunjika rasmi kwa mara nyingine tena. Baada ya uhusiano wao kuvunjika, Rashford ambaye yupo Marekani kwa mapumziko, alinaswa na kamera akiingia hotelini na mrembo mwingine ambaye hakufahamika jina. Rashford alipitia nyakati ngumu kipindi fulani baada ya kuachana na mpenzi wake huyo ambaye asili yake ni Italia.
Anaingizaje pesa
Rashford anaingiza Pauni 60 milioni kila mwaka kutokana na mshahara wa kila wiki pale Man United na mikataba mbalimbali aliyosaini katika kampuni kama Nike, EA Sports, McDonald, ambazo zinamuingizia pesa za kutosha. Vile ana miradi yake mbalimbali kama uchapishaji wa vitabu vya watoto na kila msimu anasambaza katika shule zote za jiji la Manchester.
Magari ya kifahari
Rashford anamiliki magari ya kifahari na aina mbalimbali kama Audi A3, Mercedes CLA Class, Mercedes S Class Coupe, Audi RS4 na Range Rover Velar. Gari lake la kwanza kwanza la kifahari kununua ni Audi ES4 na alinunua kwa Pauni 60,000 (sawa na Sh179 milioni) za Kitanzania.