Kylian Mbappe ametimkia zake Real Madrid na jambo hilo limeacha pengo kubwa linalohitaji kuzibwa huko Paris Saint-Germain.
Fowadi huyo Mfaransa mwenye umri wa miaka 25, amejiunga na Real Madrid kwa mkataba wa miaka mitano huku mwenyewe akifichua kwamba uhamisho huo ni ndoto iliyotimia kwa upande wake baada ya kutua Bernabeu.
Mbappe ameondoka PSG akiwa amefunga mabao 256 katika mechi 308. Na sasa mabosi wa PSG wanapambana kutafuta wachezaji wa kuja kuziba pengo lake huko Parc des Princes dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi.
Na kwenye orodha ya mastaa inaowasaka yupo mkali wa Manchester United, nyota wawili wa Napoli pamoja na mchezaji ambaye pia anasakwa na Arsenal.
Hawa hapa mastaa wanaosakwa na PSG kwa ajili ya kwenda kuziba pengo la mkali Mbappe.
-Marcus Rashford; Mwingereza Marcus Rashford atakuwa na uamuzi mkubwa wa kufanya kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi baada ya mambo yake kuwa magumu Man United. PSG inamtazama kwa jicho la matanio, wakihitaji akaongoze safu yao ya ushambuliaji Parc des Princes.
-Khvicha Kvaratskhelia; Winga huyo wa Napoli yupo kwenye rada za PSG, huku mkataba wake ukielezwa kuwa na kipengele kinachohitaji kulipwa Pauni 85 milioni kwa timu itakayohitaji huduma yake. Napoli haikuwa vizuri kwa msimu uliopita, lakini winga huyo wa Georgia, alichangia mabao 20.
-Benjamin Sesko; Kuna klabu kibao za Ligi Kuu England ikiwamo Arsenal na Man United, zinahitaji huduma ya Benjamin Sesko. Lakini, sasa PSG inamtazama kama mchezaji ambaye anaweza kwenda kuongeza kitu kwenye kikosi chao. Huduma naye inaweza kupatikana kwa Pauni 55 milioni.
-Eric-Maxim Choupo-Moting; Uhamisho ambao unaweza kushtua wengi na pengine hata nyota waliopo PSG kwa sasa, Goncalo Ramos na Randal Kolo Muani, endapo itamsajili Eric-Maxim Choupo-Moting. Staa huyo amefunga mabao tisa katika mechi 51 na saini yake haina gharama kubwa.
-Victor Osimhen; Chaguo jingine la PSG katika mchakato wao wa kuziba pengo la Mbappe ni kunasa saini ya straika wa Napoli, Victor Osimhen.
Staa huyo wa Nigeria anaweza kuuzwa kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi endapo itawekwa mezani pesa inayoanzia Pauni 113 milioni.