Meneja mpya wa Manchester United, Ralf Rangnick amekiri kuwa itakuwa vigumu sana kufanya sajili zenye tija mwezi Januari.
Mashetani Wekundu wamehusishwa na idadi ya wachezaji kabla kuelekea dirisha la usajili la majira ya baridi huku kukiwa na mapendekezo kwamba Rangnick anaweza kukabidhiwa hadi Pauni milioni 100 kuboresha kikosi.
Mchezaji wa RB Leipzig Amadou Haidara ni miongoni mwa wanaofikiriwa kuhitajika Man United, lakini kocha mkuu wa klabu hiyo amesema kuwa kwa sasa si wakati mwafaka kujadili uwezekano wa biashara Januari.
“Hatujazungumza kuhusu wachezaji wapya. Sasa ni wakati wa kukifahamu kikosi cha sasa kwa undani, kikosi hakika si kidogo”
“Kuna wachezaji wa kutosha. Labda baada ya Krismasi, kutakuwa na wakati wa kuzungumza kuhusu uhamisho unaowezekana wakati wa majira ya baridi. Kwa uzoefu wangu, majira ya baridi sio wakati wa uhamisho wenye tija. Itakuwa vigumu wakati wa baridi.”
Rangnick pia ameweka wazi kwamba alijaribu kumshawishi Michael Carrick kusalia katika klabu hiyo.