Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ranga, Yanga bado hakijaeleweka, anukia Kaizer

Ranga Chivaviro Ranga, Yanga bado hakijaeleweka, anukia Kaizer

Mon, 19 Jun 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Licha ya video iliyosambaa jana ikimuonyesha straika wa Marumo Gallats, Ranga Chivaviro akiwa na jezi ya Yanga na kuonyesha kwamba eneo alilopo ni Tanzania, taarifa za uhakika ambazo Mwanaspoti inazo ni kwamba staa huyo bado hajafika nchini na hajafikia makubaliano yoyote na Yanga kama inavyoelezwa.

Kwa mujibu wa wawakilishi wake ni kwamba Ranga bado yupo nchini Afrika ya Kusini na jezi aliyoivaa ilikuwa ni zawadi aliyopewa na mmoja ya mabeki wa Yanga baada ya mchezo wao wa marudiano wa michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika uliochezwa Afrika Kusini Mei 17 iliyoisha kwa 2-1 huku Ranga akitupia.

Awali Yanga ilionyesha nia ya kutaka kumsajili Ranga ili akawe mbadala wa Fiston Kalala Mayele ambaye huenda akaondoka katika dirisha hili kwani huduma yake inahitaji na timu nyingi barani Afrika.

Katika kuhakikisha hilo linafanikiwa rais wa Yanga Hersi Said alikutana na wawakilishi wa staa huyu wakati wameenda kucheza mechi ya marudiano kule nchini Afrika ya Kusini kwa ajili ya kujadili uwezekano wa dili kukamilika.

Lakini hakuna muafaka wowote ulifikiwa na wakala wake Trabi Harve aliliambia Mwanaspoti kwamba kinachoendelea sasa ni tetesi tu na hakuna makubaliano yoyote kati yao na Yanga.

"Ranga yupo hapa (Afrika ya Kusini), hakuna makubaliano yoyote tuliyofikia na Yanga, alivaa jezi kwa sababu ilikuwa ni zawadi aliyopewa na moja ya mabeki wa Yanga walipokutana kwenye mechi na pia alivaa (jana) kwa ajili ya kuonyesha kwamba anasapoti timu ya Taifa ya Tanzania,"

Kwa upande wa Ranga mwenyewe alisema kwamba yeye kama mchezaji angependa kucheza Tanzania kwa sababu ya vaibu la mashabiki lakini mwisho wa yote uamuzi wa wapi ataenda kucheza msimu ujao utategemeana na maslahi.

"Vaibu la mashabiki pale kwa Mkapa linafanya mchezaji yoyote kutamani kucheza mechi hapo akiwa na timu ya hapo Tanzania, hivyo hata mimi ningependa,"

Hata hivyo kwa mujibu wa vyanzo mbali mbali kutoka nchini Afrika ya Kusini ni kwamba staa huyu ameshamalizana na Kaizer Chiefs na ataichezea timu hiyo kwa msimu ujao.

Ranga ni miongoni mwa mastaa waliofanya vizuri kwa msimu uliopita kwenye michuano mbali mbali na zaidi ilikuwa kwenye Kombe la Shirikisho barani Afrika ambapo ameibuka mfungaji bora namba mbili akifunga mabao sita nyuma ya Fiston Mayele ambaye amemaliza kinara na mabao saba.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: