Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ramani ya ubingwa Yanga

Yanga DSM Ramani ya ubingwa Yanga

Fri, 30 Dec 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Azam ugenini juzi umeifanya Yanga izidi kujikita kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ikifikisha pointi 47, huku ikijiandaa kuifuata na Mtibwa Sugar Jumamosi hii kwenye Uwanja wa Manungu Complex, Turiani.

Matokeo hayo yamezidi kuongeza matumaini ya kutetea taji ililotwaa msimu uliopita bila kupoteza mechi, huku rekodi hiyo ikivunjwa msimu huu katika mchezo wa 50 ilipokubali kipigo cha mabao 2-1 kutoka kwa Ihefu Novemba 29.

Baada ya kuutafuna mfupa mgumu wa Azam, ambao duru la kwanza iliambulia pointi moja nyumbani kwa sare ya 2-2, sasa Yanga imebakiza mechi 12 sawa na pointi 36, ili kumaliza msimu nne tu kati ya hizo ikicheza nje na Benjamin Mkapa.

Kati ya michezo 12, iliyobakiza Yanga, mechi hizo nne ndizo zinaonekana kuwa na presha kubwa kwao kutokana na ushindani wa timu husika pindi zinapokutana na mabingwa hao wa kihistoria kulingana na viwanja vitakavyotumika kwa mechi hizo.

Mechi nyingine saba hazionekani kama zitakuwa ngumu sana kwa Yanga kulinganisha na hizo nne ambazo hata washindani wao wakuu Simba wanazitazama kama fursa kwao ama kuifikia au kuipiku Yanga kileleni mwa msimamo.

Mechi hizo ni dhidi ya, Mtibwa Sugar (Desemba 31), KMC (Machi 15, 2023), Singida BS (Aprili 25, 2023), Mbeya City (Mei 24, 2023) na Prisons (Mei 27, 2023).

Mbali na mechi hizo za ugenini, pia saba zilizobaki kuna mechi moja ya dabi na Simba ambao duru la kwanza zilitoka sare ya bao 1-1 Oktoba 23, huku zingine zikiwa na Ihefu (Januari 31, 2023), Ruvu Shooting (Februari 5, 2023), Namungo (Februari 14, 2023), Geita Gold (Aprili 8, 2023), Kagera Sugar (Aprili 12, 2023) na Dodoma Jiji itakayopangiwa tarehe.

Yanga imeonekana kupata ugumu inapokabiliana na timu za Mbeya, Prisons na Mbeya City ambazo msimu uliopita ziliipa ushindi.

Mechi nyingine ngumu kwa Yanga ni zile zitakazochezwa Kwa Mkapa dhidi ya Simba na Namungo.

Mechi na Namungo ni mtihani kwa Yanga kwani timu hiyo imekuwa ikiivimbia kila inapokutana nayo, kumbukumbu zikionyesha katika mechi tano zilizopita za ligi baina yao, Yanga imeshinda mara moja tu, duru la kwanza la msimu huu.

Urahisi kwa Yanga unaweza kupatikana kwa kuwepo pia kwa mechi sita ngumu kwa Simba inayochuana nao kwenye mbio za ubingwa.

Mechi hizo sita za kibabe za Simba zinazoweza kuirahisishia kazi Yanga ni za ugenini dhidi ya Azam, Mtibwa Sugar, Namungo na Ihefu pamoja na mbili za Kwa Mkapa ikiwamo dhidi ya Yanga na Singida.

Kocha wa Yanga, Nasreddine Nabi alisema malengo yao ni kutetea taji, hivyo wanaangalia michezo ijayo kwa umakini ili kupata matokeo mazuri, licha ya kukiri ugumu wa ratiba ilivyo.

“Hadi tulipofikia hatuwezi kusema tumemaliza kazi, bado tunasafari ndefu hadi mwisho wa msimu, pointi ndizo zitakazoamua, ila muhimu ni kuhakikisha timu inapambana kupata pointi katika kila mechi ijayo na tunatambua sio rahisi, ila malengo na jitihada ndizo zitakubeba,” alisema Nabi.

Kwa upande mwingine, kiraka wa timu hiyo, Yannick Bangala alisema ligi ni ngumu katika ngwe hii ya mwisho kwani, kila timu inapambana kupata matokeo mazuri ya kujiweka nafasi nzuri, japo wao kiu yao ni kutetea taji. ”Lengo letu ni kutetea taji japo si rahisi, lakini tumejipanga kupapamba,” alisema Bangala.

Chanzo: Mwanaspoti