Sshirikisho la kimataifa la vyama vya mchezo wa soka (FIFA) limetangaza majina 14 yatakayowania Tuzo ya Mchezaji Bora wa Dunia kwa mwaka 2022.
Mastaa hao ni Julian Alvarez, Jude Bellingham, Karim Benzema, Kevin de Bruyne, Erling Haaland, Achraf Hakimi, Robert Lewandowski, Sadio Mane, Kylian Mbappe, Lionel Messi, Luka Modric, Neymar, Mohamed Salah na Vinicius Junior.
Tuzo hiyo inamtambua mchezaji bora wa mwaka mzima wa 2022, ambapo Karim Benzema (mshindi wa Ballon d’Or, LaLiga na Ligi ya Mabingwa Ulaya) na Lionel Messi (mshindi wa Kombe la Dunia na Ballon d’Or) wapo kwenye vita ya kufukuzia tuzo hiyo ya Fifa.
Mgawanyo wa kura upoje?
Mchakato wa kupiga kura kupata mshindi umeanza rasmi, juzi Alhamisi na tuzo zenyewe zitatolewa Februari 27 mwaka huu. Kura zimegawanywa kwenye makundi manne, asilimia 25 inatoka kwa waandishi wa habari, asilimia 25 nyingine kutoka kwa manahodha wa timu zilizocheza Kombe la Dunia, asilimia 25 nyingine zinatoka kwa makocha na asilimia 25 iliyobaki ni kura za mashabiki.
Tuzo zitakazoshindaniwa 2022:
Ukiweka kando Tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwaka, kuna vipengele vingine 11 vitapata washindi katika sherehe hizo zitakazofanyika Februari 27. Tuzo hizo zitakazoshindaniwa ni Mchezaji Bora kwa Wanawake, Mchezaji Bora wa Wanaume, Kocha Bora kwa Wanawake, Kocha Bora kwa Wanaume, Kipa Bora kwa Wanawake, Kipa Bora kwa Wanaume, Kikosi bora kwa Wanawake, Kikosi bora kwa Wanaume, Bao Bora la Mwaka, Tuzo ya Fair Play na Tuzo ya Shabiki Bora wa Mwaka.
Wanaowania
Kwa upande wa Tuzo ya Mchezaji Bora upande wa wanawake, wanaowania: Aitana Bonmati (Barcelona), Debinha (North Carolina Courage), Jessie Fleming (Chelsea), Ada Hegerberg (Olympique Lyon), Sam Kerr (Chelsea), Beth Mead (Arsenal), Vivianne Miedema (Arsenal), Alex Morgan (San Diego Wave), Lena Oberdorf (Wolfsburg), Alexandra Popp (Wolfsburg), Alexia Putellas (Barcelona), Wendie Renard (Olympique Lyon), Keira Walsh (Barcelona) na Leah Williamson (Arsenal).
Tuzo ya Kocha bora: Carlo Ancelotti (Real Madrid), Didier Deschamps (Ufaransa), Pep Guardiola (Manchester City), Walid Regragui (Morocco) and Lionel Scaloni (Argentina), wakati makocha wa upande wa wanawake ni Sonia Bompastor (Olympique Lyon), Emma Hayes (Chelsea), Bev Priestman (Canada), Pia Sundhage (Brazil), Martina Voss-Tecklenburg (Germany) na Sarina Wiegman (England).
Tuzo ya makipa: Alisson Becker (Liverpool), Yassine Bounou (Sevilla), Thibaut Courtois (Real Madrid), Ederson (Manchester City) na Emiliano Martinez (Aston Villa), wakati kwa upande wa wanawake ni Christine Endler (Olympique Lyon), Ann-Katrin Berger (Chelsea), Mary Earps (Manchester United), Merle Frohms (Wolfsburg), Alyssa Naeher (Chicago Red Stars) and Sandra Panos (Barcelona).
Kwenye Tuzo ya Shabiki Bora wa mwaka, anayewania ni Abdullah Al Salmi (Saudi Arabia): Abdullah alitembea kukatiza jangwa kutoka kwao Jeddah hadi Qatar kwenda kuishabikia timu yake kwenye fainali za Kombe la Dunia. Mashabiki wa Argentina, ambao walionyesha nguvu kubwa kuishabikia timu yao hadi inachukua ubingwa.
Tuzo hiyo itawashirikisha pia mashabiki wa Japan, ambao wamekuwa maarufu kwa kubaki viwanjani hadi baada ya mechi kumalizika ili kufanya usafi kwenye mechi za Kombe la Dunia.