Nyota wa Biashara United, Ramadhan Chombo ‘Redondo’ ni miongoni mwa wachezaji walioitwa kuunda kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ kitakachoingia kambini kujiandaa na michezo ya kuwania kufuzu Kombe la Dunia 2022 dhidi ya DR Congo na Madagascar.
Akizungumza na wanahabari leo asubuhi kwenye chumba cha mikutano cha Shirikisho la Mpira wa Miguu (TFF), Karume Dar es Salaam, kocha mkuu wa Taifa Stars Kim Poulsen amemtaja Redondo kuwa mchezaji pekee mpya aliyeitwa kikosini kwani wengine wote walikuwepo kwenye kikosi kilichopita.
Kim amesema kuwa ubora, uzoefu na kiwango cha sasa cha Redondo ndiyo sababu kubwa ya kumuita Taifa Stars kwani anaamini ataisaidia timu hiyo katika mechi zake na DR Congo sambamba na Madagascar.
“Kila mmoja ameona namna kiwango chake kwa sasa kilivyo juu, pili ni mchezaji mwenye uzoefu ambaye ataongeza kitu ndani ya timu kuelekea mechi mbili zilizo mbele yetu,” alisema Kim.
Pamoja na Redondo, wengine walioitwa ni Aishi Manula (Simba), Metacha Mnata (Polisi Tanzania), Ramadhan Kabwili (Yanga), Shomari Kapombe (Simba), Kibwana Shomari (Yanga), Israel Mwenda (Simba) na Mohamed Hussein( Simba).
Wengine ni Erasto Nyoni (Simba), Dickson Job (Yanga), Bakari Mwamnyeto (Yanga), Kennedy Juma (Simba), Lusajo Mwaikenda (Azam), Edward Manyama (Azam), Nickson Kibabage (KMC), Meshack Mwamwita (Kagera Sugar), Novatus Dismas (Maccabi Tel Aviv - Israel) na Mzamiru Yassin (Simba).
Zawadi Mauya (Yanga), Feisal Salum ( Yanga), John Bocco (Simba), Iddy Seleman (Azam), Abdul Seleman (Coastal Union), Mbwana Samatta (Royal Antwerp -Ubelgiji), Kibu Denis (Simba), Reliants Lusajo (Namungo) na Simon Msuva (Wydad AC- Morocco) nao pia wameitwa.
Taifa Stars inatarajia kucheza mechi ya marudiano na DR Congo, Novemba 11 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa baada ya kutoa sare ya bao 1-1, ugenini kisha itasafiri kwenda Madagascar kucheza mchezo wa marudiabo utakaopigwa Novemba 14, baada ya kushinda nyumbani 3-2, Septemba mwaka huu.