Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Rais wa Fifa aigomea kadi ya bluu

Kombe La Dunia Limekuwa Bora Zaidi Kuwahi Kushuhudiwa   Infantino Rais wa FIFA, Gianni Infantino

Mon, 4 Mar 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Shirikisho la vyama vya mpira wa miguu duniani (Fifa), limesema haliungi mkono wazo la kuanzishwa kwa kadi ya bluu ambalo limekuwa likipigiwa chapuo na bodi ya kimataifa ya chama cha soka (Ifab), tangu mwanzoni mwa mwaka huu.

Rais wa Fifa, Gianni Infantino amesema kuwa Fifa haioni umuhimu na maslahi ya kadi ya bluu katika maendeleo ya mchezo wa mpira wa miguu hivyo haitokuwa tayari kuunga mkono kuanzishwa na matumizi yake.

"Fifa inapingana na pendekezo la bodi ya kimataifa ya chama cha soka la kinachoitwa kadi ya bluu. Sikuwa nafahamu kitu kama hicho hadi nilipoona kimeteka hisia za wengi," alisema Infantino.

Inaripotiwa kuwa ujumbe wa Fifa umepanga kuhakikisha suala la kadi ya bluu halifanikiwi katika mkutano mkuu wa mwaka wa Ifab unaoendelea Scotland kujadili mabadiliko na maboresho ya vipengele tofauti vya sheria 17 za mpira wa miguu duniani.

Katika mkutano huo ambao uamuzi wa mwisho hufanywa kwa upigaji wa kura, Fifa huwakilishwa na wajumbe wanne na Ifab nayo inawakilishwa na idadi kama hiyo ya wajumbe na iwapo kuna hoja kinzani, upande ambao hupata kura nyingi ndio uamuzi wake hupitishwa.

Fifa inaripotiwa kuandaa jopo la wataalam wa sheria ambao watatumika kushawishi wajumbe kukataa mpango wa uanzishwaji wa kadi hiyo ambayo mastaa wengi wakubwa soka duniani wameonekana kutounga mkono uanzishwaji wake wakidai utaziathiri timu na ladha ya soka na miongoni mwao ni kocha wa Liverpool, Jurgen Klopp.

Lengo la Ifab kuanzisha kadi ya bluu ni kujaribu kupunguza kasi ya wachezaji kucheza rafu na kufanya makosa ya utovu wa nidhamu, hasa utoaji wa lugha chafu na kubishia uamuzi wa refa.

Kwa mujibu wa ufafanuzi wa Ifab, katika matumizi ya kadi hiyo, wachezaji watakuwa wakitolewa uwanjani kwa dakika 10 kama watafanya madhambi makubwa au kupinga uamuzi wa marefa. Mchezaji anayeonyeshwa kadi ya bluu, hutolewi moja kwa moja, anakuwa amewekwa kwenye “kapu la watenda madhambi” nje ya uwanja kwa dakika 10, kisha unarudishwa mchezoni.

Tayari kadi hiyo ilishaanza kufanyiwa majaribio katika ligi za madaraja ya chini, za vijana na mashindano ya ridhaa ya soka England na Wales ambazo ni miongoni mwa wajumbe wanne wa Ifab ingawa hayakugusa madaraja ya juu ya ligi.

Mbali na mjadala kuhusu kadi ya bluu, mkutano huo mkuu wa Ifab pia utajadili na kutolea uamuzi pendekezo la kutoa mamlaka kwa refa kusimamisha rasmi mchezo kwa ajili ya kuwapa nafasi wachezaji kunywa maji ili kutotoa nafasi kwa timu moja kunufaika au kuathirika kutokana na tukio hilo.

Hiyo itakuwa ni tofauti na utaratibu wa sasa ambao refa hana muda maalum wa kusimamisha mchezo kwa ajili ya wachezaji kupooza miili, jambo ambalo linaweza kusababisha baadhi ya wachezaji kuchelewa kurejea uwanjani.

Chanzo: Mwanaspoti