Rais wa Shirikisho la Soka ulimwenguni (FIFA), Gianni Infantino amekosolewa vikali kwa baada ya kupiga picha ‘Selfie’ karibu na Jeneza la aliyekuwa Gwiji wa Soka ulimwenguni, Pele aliyefariki dunia wiki iliyopita.
Infantino alikuwa mmoja wa watu mashuhuri katika Mazishi ya Gwiji huyo wa Brazil siku ya Jumatatu, lakini baadhi ya watu walimkosoa kwa kitendo cha kupiga picha ‘selfie’ mbele ya Jeneza, hali iliyopelekea kuzua mijadala kufuatia tukio hilo.
Picha hiyo ilionyesha Rais huyo akitabasamu kwa utulivu pamoja na watu wengine waliohudhuria mazishi hayo, huku wakiwa umbali wa mita chache kutoka kwenye Jeneza la Gwiji huyo.
Rais huyo wa FIFA baada ya kifo cha Pelé alinukuliwa akisema, angependa Mataifa yote ambayo ni Wanachama wa FIFA yawe na angalau uwanja mmoja katika nchi zao uliopewa jina la Pele ili urithi wake ukumbukwe na vizazi vya sasa na baadae katika kumuenzi Gwiji huyo.