Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Rais ZFF afyekwa uchaguzi

IMG 4449.jpeg Rais ZFF afyekwa uchaguzi

Sun, 25 Jun 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka Zanzibar (ZFF) imewapitisha wagombea watatu nafasi ya urais, huku Rais wa sasa Abdulatif Ali Yassin naye akifyekwa kwenye kinyang'anyiro hicho kitakachofanyika Julai 8 visiwani hapa.

Kamati hiyo imeweka hadharani majina hayo baada ya kukamilika kwa usaili uliwashirikisha wagombea saba na watatu kati yao ndipo wakapitishwa huku wanne wakikatwa.

Akitoa taarifa kwa niaba ya kamati hiyo ya uchaguzi, Ofisa Habari na Mawasiliano wa ZFF, Mohammed Kabwanga alisema wagombea waliopita ni wale waliokidhi vigezo kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi wa ZFF na wale waliokatwa hawakukidhi vigezo.

Akiwataja wagombea watatu waliopita ni Suleiman Mahmoud Jabir, Kamal Abdul Satar, Juma Hassan Thabit na waliokatwa kwa kukosa vigezo ni Abdulatif Ali Yassin, Rajab Ali Rajab, Nasra Juma Mohammed na Mwinyi Khalid Thabit.

Kabwanga alisema wagombea hao waliokatwa majina yao wanayo haki ya kuwekewa pingamizi na kukata rufaa ikiwa hawakuridhishwa na maamuzi hayo huku akisema majina ya wagombea waliopitiswa ni ya hatua ya awali tu .

"Kamati inasisitiza kuwa majina haya ambayo wameyatoa ni majina ya awali bado kamati inaendelea kufuatilia matendo na mienendo ya wagombea wote na endapo watajiridhisha kuwa mgombea amepoteza sifa basi ataondoshwa", alisema Kabwanga.

Rais wa ZFF, hakupatikana kufafanua kilichomkuta na kama ana nia ya kukata rufaa licha ya kuzua maswali ilikuwaje uchaguzi uliopita alichaguliwa na safari hii akatwe, japo Mwenyekiti wa Kamati ya uchaguzi huo, Fadhil Ramadhan Mberwa alisema kila aliyekatwa amepewa sababu kupitia barua walizotumiwa wahusika.

Uchaguzi wa nafasi ya Urais wa Shirikisho la mpira wa miguu Zanzibar (ZFF) unatarajiwa kufanyika Julai nane mwaka huu, wakati kampeni zitaanza Juni 30.

Chanzo: Mwanaspoti