Rais wa Klabu ya Young Africans Injinia Hersi Said amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwa kutimiza ahadi yake.
Rais Samia aliahidi kununua kila bao kwa Shilingi Milioni Tano kabla ya michezo ya Kimataifa ya CAF iliyochezwa mwishoni mwa juma lililopita, kwa kuzihusisha Young Africans na Simba SC.
Injinia Hersi amesema hawana budi kumshukuru Rais Samia kwa kutekeleza ahadi yake, na wao kama Young Africans wametekeleza kwa vitendo kufuatia ushindi wa 3-1 dhidi ya TP Mazembe jana Jumapili (Februari 19), Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.
Hata hivyo Kiongozi huyo amesema mbali na ahadi ya Rais Samia, pia Wadau wengine ambao hakuwataja, wamechangia kiasi cha fedha kufuatia kufurahishwa na ushindi wa Young Africans kwenye mchezo huo wa Kombe la Shirikisho Barani Afrika.
“Tumetekeleza maagizo ya Muheshimiwa Rais, Rais hawezi kutoa zawadi halafu ikabaki ina hang hang, tunamshukuru sana Mama yetu Rais Samia Suluhu Hassan, tumetekeleza maelekezo yake.”
“Zimeongezeka, zile Milioni Kumi na Tano za Muheshimiwa Rais, wadau wengine wameongeza, kwa hiyo tunashukuru Mwenyezi Mungu kwa kusema Alhamdulillah.” amesema Injinia Hersi Said
Kwa ushindi wa 3-1, Young Africans imekabidhiwa Shilingi Milioni Kumi na Tano za Rais Samia, ambazo zilikabidhiwa na Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa baada ya mchezo huo, Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.