Rais wa Klabu Bingwa Tanzania Bara Young Africans, Hersi Said amesema wachezaji wa timu hiyo walionesha kiwango bora kwenye mchezo wa Robo Fainali wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Manelodi Sundows na kwamba hakuna mtu anayewadai.
Kwenye mchezo huo Young Africans walifungwa kwa mikwaju ya Penati 3-2 kufuatia sare ya bila kufungana dakika 90 za mchezo huo katika Uwanja wa Loftus Versfeld, Pretoria, Afrika Kusini na kutolewa kwenye mashindano hayo.
Katika mchezo huo mwamuzi Dahana Belda kutoka Mauritania aliwanyima Young Africans bao lililofungwa kwa shuti kali na kiungo mshambuliaji wa timu hiyo Stephan Aziz Ki na mpira kugonga mwamba wa juu na kuangukia ndani.
Hata hivyo mwamuzi huyo alitafisiri kuwa mpira huo haukuingia ndani moja kwa moja na wala hakwenda kufanya marejeo ya video na kulikataa bao hilo.
Akizungumza na wachezaji wa timu hiyo kweye vyumba vya kubadilishia nguo baada ya mchezo huo Hersi alisema hakuna mtu anayewadai wachezaji hao kutokana na kiwango bora walichoonesha kwenye mchezo huo na kwamba wanaweka mkazo kwenye Kombe la Shirikisho la CRDB na Ligi Kuu Soka Tanzania Bara.
“Wachezaji tuanze kwa kumshukuru Mungu, ilikuwa siku nzuri, tumecheza mchezo wa Robo Fainali kwa kiwango kizuri, kila mmoja ana furaha, kila mmoja ameridhishwa na kiwango chenu, tumekwenda kwenye matuta eneo ambalo Mungu hakutupangia.”
“Hakuna mtu tunayemdai hapa, hakuna, kila mmoja kwa nafasi yake alikuwa na mchango mkubwa kwenye mchezo wa Dar es salaam na wa Pretoria na timu inayotaka mafanikio inacheza hivi, lakini mchezo huu umeamuliwa kwa bahati na dhuluma kila mmoja ameona,” amesema Hersi.
Amesema hatua hiyo ndio Mungu aliyowaandikia kwenye michuano ya kimataifa lakini msimu hajauisha wanatakiwa kurudi nyumbani kwani wana mechi ya kounbe la Shirikishi la CRDB Aprili 10 na mechi ya ligi Aprili 14, hivyo lazima wachukue ubingwa wa ligi waweze kurudi tena kimataifa.