Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Rais TLS ataja chanzo mkwamo Katiba mpy

Sungusia TLS Wakili Harold Sungusia.

Mon, 24 Jun 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Wakili Harold Sungusia, amesema moja ya chanzo kikubwa cha kuchelewesha mchakato wa upatikanaji wa Katiba mpya ni pamoja na mgongano wa maslahi.

Aidha, kikwazo hicho kimesababisha msimu uliopita kushindwa kufanyia kazi maoni kuhusu mchakato wa Katiba mpya, yaliyotolewa na wananchi pamoja na wadau mbalimbali.

Wakili Sungusia amesema hayo jijini Dodoma wakati akifungua mkutano wa wadau kutoa maoni yao kuhusu mchakato wa Katiba mpya.

Amesema safari hii TLS wamejipanga kuhakikisha maoni waliyochukua katika mikoa mitano yanafanyiwa kazi ili  mchakato huo ukamilike.

Amebainisha mambo matatu ambayo wameyagundua kwa wananchi na baadhi ya viongozi kuhusu Katiba iliyopo sasa kwa mikoa ambayo wamefanya mikutano.

Kwa mujibu wa Wakili Sungusia, kuna makundi matatu ambayo ni; wanaosema “Katiba ya sasahivi haina tatizo lolote tusipoteze muda tuendelee na maisha yetu”.

Kundi la pili ni wale wanaosema “Katiba iliyopo ina dosari kadhaa ambazo tunaweza kuzirekebisha tukaenda mbele” na kundi la tatu ni “wanaosema Katiba iliyopo haifai kabisa inahitajika katiba mpya ambayo itasaidia nchi kwenda mbele”.

"Wananchi wana maoni mengi, lakini ukisikiliza kwa haraka utagundua kwamba wamesikitishwa na kilichotokea mwaka 2014 baada ya ile Tume ya Katiba iliyokuwa ikiongozwa na Jaji Joseph Warioba kumaliza kazi yake," amesema. Aidha, miongoni mwa mambo ambayo wamejiuliza ni kwanini mchakato uliopita ulikwama.

"Usipojua ulipoangukia na kilichokusababisha ukaanguka, huwezi kuchukua tahadhari kwa hatua unazoenda mbele, tulikwama kwenye mchakato uliopita kwa sababu ya mgongano wa maslahi, waliokuwa nje ya utawala walidhani kwamba watatumia katiba kuweza kuingia madarakani na waliokuwa madarakani walidhani watatumia mchakato wa katiba kuendelea kubaki madarakani," amesema.

"Sisi tunataka Katiba ya wananchi sio Katiba ya makundi fulani katika nchi hapana, ni Katiba ya raia wote wajisikie Katiba ni ya kwao kwa utaratibu huo tunapendekeza mchakato utakaofuata wakupata katiba ya wananchi usimamie umahiri wake," amesema.

Pia, watakaohusika katika kuandaa mchakato wa katiba wasihusike katika kugombea nafasi zozote za kisiasa.

MAUAJI WENYE UALBINO Katika hatua nyingine, Wakili Sungusia amezungumzia suala la mauji ya watu wenye ualbino yanayoendelea nchini amesema kuwa TLS inakemea kwa nguvu zote. Amesisitiza kuwa kamwe Watanzania wasikubali jambo hilo liendelee na kutoa wito kwa taasisi zote kuchukua hatua kukemea hayo mauaji.

Inock Isaya, akizungumza katika mjadala huo, amesema kuwa Katiba itakayopendekezwa iwazingatie watu wote wenye ulemavu wa aina tofauti.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live