Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Rais TFF: Serengeti Girls inaweza kutinga Nusu Fainali

Wallace Karia Rais wa TFF, Walace Karia

Wed, 19 Oct 2022 Chanzo: dar24.com

Rais wa Shirikisho la soka Tanzania ‘TFF’ Wallace Karia amewataka wachezaji wa Timu ya Taifa ya Wanawake chini ya umri wa Miaka 17 ‘Serengeti Girls’, kuamini wanaweza kuifunga Colombia kama walivyofanya kwa Ufaransa na baadae kulazimisha sare dhidi ya Canada.

Serengeti Girls itacheza dhidi ya Colombia katika mchezo wa Robo Fainali, Kombe la Dunia Jumamosi (Oktoba 22), baada ya kutinga hatua hiyo, kufuatia matokeo ya sare ya 1-1 dhidi ya Canada ilioyapata jana Jumanne (Oktoba 18) nchini India zinapoendelea Fainali hizo.

Akizungumza na Azam TV nchini India, Karia amesema baada ya mchezo dhidi ya Canada, alikutana na Kikosi cha ‘Serengeti Girls’, kwa ajili ya mazungumzo na ndipo alipowasisitiza kuendelea kupambana, kwani ana uhakika wana uwezo wa kuifunga Colombia.

“Naamini wanaweza kupambana na wakashinda mchezo dhidi ya Colombia, kama ilivyokua kwa Ufaransa ambayo ilipewa nafasi kubwa ya kuifunga Tanzania lakini haikuwa hivyo, pia wamelazimisha sare dhidi ya Canada, pia ‘Serengeti Girls’, haikupewa nafasi ya kufanya hivyo.”

“Tunafahamu Colombia ipo juu kimpira kuliko Tanzania, lakini nilichowaambai mabinti wanakwenda kucheza na Mabinti wenzao chini ya miaka 17, hivyo hakuna kitakachowashinda katika mchezo huo zaidi ya kupambana na kuhakikisha wanashinda.” amesema Karia

Katika hatua nyingine Rais wa TFF Wallace Karia, amewashukuru Wadau wa Soka nchini Tanzania kwa kuendelea kuwa pamoja na ‘Serengeti Girls’, katika kipindi hiki ambacho inapambana kwenye Fainali za Kombe la Dunia huko India.

“Nafahamu Watanzania wanaiombea timu yao, wako pamoja na timu hii na wanaitakia mema kila inapokua katika majukumu yake ya kuitetea nchi, kwa hilo ninawashukuru na kuwasisitiza waendelee kufanya hivyo kwa sababu hii sio timu ya TFF ni timu ya watanzania.” amesema Karia

Colombia inakutana na Serengeti Girls, baada ya kuongoza Kundi C ikiwa na alama sita sawa na Mabingwa watetezi Hispania iliyozidiwa uwiyano wa mabao ya kufunga na kufungwa.

Michezo mingine ya Robo Fainali Kombe la Dunia kwa Wanawake chini ya umri wa miaka 17, itashuhudia Marekani ikicheza dhidi ya Nigeria Oktoba 21 katika Uwanja wa DY Patil mjini Mumbai, huku siku hiyo hiyo Ujerumani itaikabili Brazil.

Kikosi cha Japan kitacheza dhidi ya Mabingwa watetezi Hispania Oktoba 22 katika Uwanja wa Pandit Jawaharlal Nehru mjini Margao, ambao pia utashuhudia Tanzania ikipapatuana na Colombia siku hiyo.

Chanzo: dar24.com