Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk Samia Suluhu amesema kuwa Serikali imedhamiria kuwa wenyeji wa Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika 2027, hivyo watajenga viwanja viwili kuimarisha miundombinu.
Hayo aliyasema jana Jumapili (Agosti 06) alipokuwa mgeni rasmi kwenye Tamasha la Simba Day lililofanyika Uwanja wa Mkapa, Dar.
Rais Samia amesema wamepata taarifa kuhusu wakaguzi wa miundombinu wakieleza kuwa kila kitu kinakwenda sawa jambo linaloongeza nafasi ya kuwa wenyeji wa AFCON 2027.
“Tuna mpango wa kuwa wenyeji wa AFCON 2027 kwa kushirikiana na Kenya, Uganda. Mpaka sasa tumefikia hatua nzuri na tumedhamiria kujenga viwanja viwili Arusha na Dodoma vyenye uwezo wa kuchukua watu 30,000.
“Ninafurahi kuwa kwenye tamasha la Simba Day ninatambua kuwa hili ni la 15 tokea lilipoanzishwa 2009. Nasema haya nikijua kuwa taifa zima linafuatilia ikiwa ni pamoja na watani zenu wa jadi Yanga.
“Nimewafuatilia namna ambavyo mmefanya mengi ikiwa ni pamoja na kuutangaza utalii kwa kupeleka kibegi Mlima Kilimanjaro.
Kibegi kimeitangaza Tanzania ni ubunifu ambao haujapata kutokea. Ningependa kuuliza swali kibegi kimeshuka ama bado kipo juu mlimani? Kama bado kipo mlimani basi iwe ni ajira kwa wengine kukifuata huko mlimani.”
Wakati huo huo Rais Samia amezitaka Klabu za Simba SC na Young Africans kuungana kwenye michuano ya kimataifa.
“Kwa msimu ujao niwaombe timu zote mnaoshiriki michuano ya kimataifa mshirikiane vyema na lengo likiwa ni kuhakikisha kuwa taifa linafanikiwa kimataifa,” alisema Rais Samia ambaye aliongeza kuwa ahadi yake ya kununua mabao kwenye michuano ya kimataifa itaendelea.