Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amewashukuru Simba SC kwa mwaliko wa kuhudhuria kilele cha Tamasha la "Simba Day" Agosti 6 katika Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam.
Katika Sherehe hizo Rais Samia alialikwa kama mgeni rasmi.
Kupitia kurasa zake za mitandao ya Kijamii Rais Samia ameandika;
Ahsanteni wana Simba kwa kunialika kushiriki nanyi katika siku yenu muhimu hii leo. Hongereni kwa siku nzuri. Pongezi kwenu kwa kuendelea kutangaza utalii wa nchi yetu kwa kufikisha kibegi katika kilele cha Mlima Kilimanjaro. Michezo inatuleta pamoja, inatupa burudani, na kudumisha amani na utulivu, lakini pia inachagiza katika kukuza uchumi wa nchi yetu.
Tumekuwa na mwamko na mafanikio makubwa katika michezo miaka ya karibuni. Mbali na Klabu ya Yanga kutinga fainali za Kombe la Shirikisho; Tembo Warriors, Kilimanjaro Queens na Serengeti Girls wametuwakilisha vyema kimataifa. Ahadi yangu ya hamasa ya kununua kila goli katika mashindano ya kimataifa itaendelea.
Mbali na Serikali kuendelea kuwekeza katika michezo, natoa wito pia kwa sekta binafsi kufanya hivyo. Nchi yetu ina mazingira mazuri ya kufanya biashara, na michezo ni moja ya eneo muhimu kiuwekezaji.