Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan ameipongeza sekondari ya Fountain Gate ya Dodoma kwa kutwaa ubingwa wa michuano ya shule za sekondari Afrika kwa wasichana jana Jijini Durban, Afrika Kusini.
"Nawapongeza Timu ya Wasichana ya Mpira wa Miguu ya Sekondari ya Fountain Gates Dodoma, kwa kutwaa ubingwa kwenye Mashindano ya Soka kwa Shule za Sekondari ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF African Schools Continental Champions), upande wa wasichana,".
Rais Dk. Samia amesema ushindi huo unakwenda sambamba na nia ya Serikali yake kuendelea kuboresha mtaala wa elimu nchini katika kukuza si tu elimu ya darasani, bali na vipaji pia, ili kupata wahitimu wengi zaidi wenye uwezo wa kutumia maeneo hayo mawili muhimu kuleta maendeleo.
Jana Fountain Gate ilitwaa ubingwa wa michuano ya shule za sekondari Afrika kwa wasichana baada ya ushindi wa 3-0 dhidi ya Ecole Omar IBN Khatab ya Morocco Uwanja wa King Zwelithini Jijini Durban, Afrika Kusini.
Katika michuano hiyo inayoandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF), mabao ya Fountain Gate yalifungwa na Winfrida Hubert mawili na Irene Chitanda moja na huo ulikuwa mchezo wa pili jana baada awali kuitandika SCG De Mfilou ya Kongo mabao 4-0 katika Nusu Fainali.
Kwa kutwaa ubingwa huo, Fountain Fate imezawadiwa dola za Kimarekani 300,000, kiasi ambacho pia amepewa bingwa wa upande wa wavulana, huku washindi wa pili wakiondoka na dola 200,000 na wa tatu dola 150,000.