Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Rais Samia aongeza mzuka Stars wakiikabili Uganda, atoa tiketi 7000

Taifa Stars DUWA 1140x640 Wachezaji wa Taifa Stars

Sun, 26 Mar 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ametoa tiketi 7000 kwa ajili ya mashabiki watakaohudhuria mchezo wa kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) kati ya wenyeji 'Taifa Stars' dhidi ya Uganda utakaopigwa Jumanne hii kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa saa 1:00 usiku.

Akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Saidi Yakubu amesema tiketi hizo ni kwa ajili ya motisha ili kuhakikisha timu yetu ya taifa inafanya vizuri.

"Tunashukuru sana jitihada za Rais wetu katika maendeleo ya michezo hapa nchini, tunaamini kwa umoja huu uliopo tutafikia malengo yetu tuliyojiwekea ya kuona tunapiga hatua."

Aidha Yakubu aliongeza mbali na tiketi hizo ila wadau wengine mbalimbalj wamejitolea kwa lengo la kuhakikisha mashabiki wanajitokeza kwa wingi uwanjani ili kutoa sapoti kwa timu yao.

"Tunamshukuru pia Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa kwa kutoa tiketi 2000 na sisi kama Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo tunatoa 11, 000 na wale wote ambao wamejitoa ingawa hawakutaka kutajwa majina yao wazi," amesema.

Kwa upande wa Rais wa TFF, Wallace Karia ameipongeza Serikali chini ya Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwa juhudi kubwa inazozifanya kwa ajili ya maendeleo ya soka letu hapa nchini.

"Tunatambua changamoto kidogo zilizopo hasa katika kipindi hiki cha mfungo wa mwezi Mtukufu wa Ramadhan lakini naamini Watanzania watajitokeza kwa wingi ili kuipa timu yetu hamasa." amesema Karia. Aidha Karia aliwapongeza wachezaji na benchi la ufundi kwa kucheza soka safi na kupata ushindi wa bao 1-0 kwenye mechi dhidi ya Uganda iliyochezwa Machi 24 nchini Misri.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live