Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Rais Samia amlilia Pele, atuma salamu za pole Brazil

Pele Rais Samia amlilia Pele, atuma salamu za pole Brazil

Fri, 30 Dec 2022 Chanzo: Mwananchi

Rais Samia Suluhu Hassan leo Desemba 30, ametuma salamu za rambirambi kwa Rais wa Brazil, Jair Bolsonaro kufuatia kifo cha aliyekuwa mchezaji nguli wa mpira wa miguu wa nchi hiyo Edson Arantes do Nascimento ‘Pele’ aliyefariki jana akiwa na umri wa miaka 82.

Taarifa za kifo cha mwanasoka huyo mwenye rekodi ya kushiriki kombe la dunia mara nne na kushinda mara tatu akiwa na timu yake ya Brazil, ilithibitishwa jana na binti yake Kely Nascimento kwenye mtandao wake wa Instagram.

Rais Samia kupitia mitandao yake ya kijamii aliandika ”Nimepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha Mwanasoka wa Karne kutoka Brazil, Edson Arantes do Nascimento “Pelé”.

Mchango wake katika soka duniani utakumbukwa daima. Pole kwa Rais wa Brazilfamilia & mashabiki wote wa soka. Mungu amweke mahali pema peponi, amina,” ameandika Rais Samia.

Rais Samia anaungana na wanasiasa wengine duniani akiwamo Rais wa Kenya, William Ruto na Rais wa Marekani, Joe Biden, wanasoka na wapenzi wa soka kuomboleza kifo cha gwiji huyo.

Pele ataendelea kusalia kwenye vitabu vya historia ambapo katika miaka 1958, 1962 na 1970 alichukua Kombe la Dunia huku akibaki kinara wa ufungaji wa timu ya taifa akiwa na mabao 77 katika mechi 92.

Gwiji huyo wa soka kwa zaidi ya miaka 60 sasa ameendelea kutawala kwenye vinywa vya wanasoka duniani kutokana na rekodi yake ya kipekee ya kushinda Kombe la Dunia mara tatu.

Mara zote Pele wakati wa karia yake ya soko amesema “Nimezaliwa kucheza mpira wa migu, kama ilivyo kwa Beethoven ambaye alizaliwa kuandika muziki na Michelangelo aliyezaliwa kupaka rangi.”

Kabla ya umauti kumfika Pele alikuwa amelazwa hospitali akisumbuliwa na saratani ya utumbo.

Chanzo: Mwananchi