Rais wa Shirikisho la Soka nchini Tanzania ‘TFF’ Wallace Karia, amezipongeza Klabu za Simba na Young Africans kwa kufanikiwa kutinga hatua ya Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, akisema wameipa sifa nchi, na kwalke binafsi wamemheshimisha mbele ya viongozi wa mashirikisho mengine Afrika na dunia lakini akitoa siri ya mafanikio hayo.
Kwa mara ya kwanza katika historia ya michuano hiyo, timu za Simba na Young Africans zimetinga kwa pamoja hatua ya Robo Fainali huku Tanzania ikiwa nchi pekee iliyoingiza timu mbili katika hatua hiyo.
Mara nyingi imezoeleka kuona nchi za Kaskazini maarufu nchi za Kiarabu hususan Misri, Morocco na Tunisia zikiingiza timu mbili katika hatua hiyo, lakini safari hii ni Tanzania pekee iliyofanikiwa kufanya hivyo.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Karia, amesema hayo yote yametokana na kuigeuza ligi ya Tanzania kutoka kuwa ya ridhaa na kuwa ya kulipwa na ya kibiashara zaidi, hali iliyosababisha kuja kwa wachezaji wengi wa kigeni na wenye ubora mkubwa.
“Nazipongeza Klabu Simba na Young Africans, kuanzia viongozi na wachezaji wao, kuingia kwao hatua ya Robo Fainali kumeiheshimisha za nchini yetu, ni Tanzania pekee iliyoingiza timu mbili msimu huu, wameniheshimisha mimi kama Rais wa TFF mbele ya viongozi wenzangu na Mashirikisho ya Soka Afrika na duniani kwa jumla.
“Pia napeleka pongezi zangu kwa wachezaji wa kigeni wa Simba na Young Africans kwani wamezifikisha timu hizo hapo na wamewabadilisha hata wachezaji wetu wazawa.”
Amesema awali walipoweka idadi ya wachezaji 12 wa kigeni walipata upinzani mkali kutoka kwa baadhi ya wadau wa michezo, lakini kwa sasa Kitanzania,” alisema Karia. matunda yake yanaonekana.
“Tuliruhusu wachezaji 12 wa kigeni ili mradi tu tukaweka vigezo wawe wa viwango gani, tulipata upinzani mkali, lakini leo tunaona, ni hao hao kwa kiasi kikubwa wamezisaidia timu hizi za Tanzania ambapo sidhani kama tungekuwa na Watanzania watupu tungeweza.
“Lakini hawa wachezaji wa kigeni wamesaidia hata kuwaimarisha wachezaji wetu kwa sababu kila wiki wanacheza nao hapa kwenye ligi, kwa hiyo hata wakichaguliwa kwenye timu ya taifa wanakuwa hawana woga nao kwa kuwa wamewazoea,” amesema Karia.
Amekumbushia michuano ya AFCON 2023 iliyoisha hivi karibuni nchini Ivory Coast, ambapo Tanzania ilikuwa kwenye kundi moja na Zambia, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo na Morocco kuwa Taifa Stars haikufanya vibaya sana na nusura iende hatua ya 16 bora, kwa sababu Stars, ilikuwa kundi lenye timu zenye wachezaji wanaowafahamu.
“Wachezaji wetu waliihofia Morocco tu, lakini siyo Zambia kwa sababu ilikuwa na wachezaji wanaocheza nao kila wiki (Clatous Chama na Kennedy Musonda), na DR Congo (Henock Inonga), na hiyo ndiyo faida ya kuwa na wachezaji wa kigeni, inawaimarisha hata wachezaji wa Kitanzania kwenye timu yetu wa Taifa Stars,” amesema.
Aidha, aliwapongeza pia wadhamini mbalimbali wa ligi ambao wataonyesha mechi zote 240 za Ligi Kuu, akisema hayo ni maendeleo makubwa ya soka kipindi cha uongozi wake, ambapo sasa wachezaji wa timu zote 16 za Ligi Kuu na wa chini ya miaka 20 wanalipwa mishahara.