Kiongozi wa zamani wa Simba na soka la Tanzania, Ismail Aden Rage, amesema timu nyingi za soka nchini zimekuwa zikitumia muda mwingi kuuchezea mpira na kupigiana pasi nyingi kuliko kushambulia kwa ajili ya kutafuta mabao.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Rage ameonyesha kushangazwa na hali hiyo, akisema kwa sasa timu nyingi zimeonekana kusaka zaidi pointi nyingi za umiliki wa mpira badala ya kutafuta mabao.
Aliongea maneno hayo muda mfupi tu baada ya kutoka kutazama mechi kati ya Yanga dhidi ya Ruvu Shooting.
Kwenye mechi hiyo Yanga iliibuka na ushindi wa bao 1-0 lililowekwa wavuni na Mpoki Mwakinyuke ambaye alijifunga mwenyewe.
Rage alisema kwenye mechi hiyo, Yanga ingeweza kupata mabao mengi zaidi, lakini walitumia muda mrefu kuremba mpira, akishangaa kuwa siku hizi imekuwa ni tabia ya timu nyingi za Ligi Kuu.
"Wamejitafutia wenyewe, wala Yanga isingeshinda bao moja, wametumia muda mwingi kuuchezea mpira badala ya kushambulia moja kwa moja.
"Kama wangeshambulia moja kwa moja nadhani wangepata na hiyo nimeona ni udhaifu wa timu nyingi kwa sasa hapa Tanzania, wamekuwa wakiiga mpira wa kupasiana sana mpira kwa pasi ambazo hazina sababu za msingi badala ya kufanya mashambulizi, ili wapate pointi nyingi kwenye kuumiliki mpira.
"Utaona timu inakwenda mbele halafu ghafla utaona wanarudisha tena mpira nyuma, sasa huo siyo mpango mzuri hata kidogo kama timu inataka ushindi," alisema Rage ambaye amewahi kuongoza soka kwenye chama cha soka nchini (FAT), ambapo kwa sasa ni Shirikisho la Soka Nchini (TFF).
Alichokisema Rage ndicho ambacho kinaonekana kutaka kubadilishwa na Kocha Mkuu wa sasa wa Simba, Roberto Oliveira, ambaye anaonekana kutaka kikosi chake kucheza soka la kushambulia moja kwa moja na kwa kasi, badala ya kukaa na mpira muda mrefu wachezaji wake wakipasiana na kupiga pasi nyingi za nyuma.