Mwenyekiti wa zamani wa Klabu ya Simba SC, Ismail Aden Rage ameikumbusha Bodi mpya ya Simba Sports Club kushughulikia mambo mawili makubwa mbayo wanasimba wanatamani kuona yanakamilika.
"Waingie pale waelewe kwamba kuna mambo mawili makubwa lazima wayafanye. Moja wanachama wengi hawana imani na katiba ya Simba, kwa hiyo lazima waende wakairekebishe."
Rage ameongeza "Pili 'transformation' imechukua muda mrefu sana kwa hiyo wanachama hawajui Klabu yao inakwendaje, katika muundo gani hii imechukua miaka minne sasa."
"Kwa hiyo hivi ni vitu ambavyo Bodi mpya inatakiwa ikae iangalie na iongee na watu ambao wapo kwenye klabu yao wanaojua vizuri ili waweze kuwasaidia wanachama wakaelewa wanaelekea wapi."
Aden Rage ambaye pia amewahi kuwa kiongozi wa Shirikisho la soka Tanzania TFF kwa wakati huo FAT, amewataka wanasimba kuwapa muda viongozi hao waliyoteuliwa ili kutimiza majukumu yao na pale watakapokosea basi ni haki yao kikatiba kukosoa.