Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Rage: Pablo apewe muda

Pablo 5 Rage: Pablo apewe muda

Thu, 11 Nov 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

ALIYEWAHI kuwa Mwenyekiti wa Simba, Aden Rage amewaonya mashabiki na viongozi wa timu hiyo kuwa wasiwe na presha ya kizamani kwani mafanikio huja polepole.

Kauli ya Rage inakuja baada ya timu hiyo kumtangaza kocha Pablo Franco aliyechukua nafasi ya Didier Gomes aliyetimuliwa Oktoba 26 baada ya kuondoshwa Ligi ya Mabingwa Afrika na Jwaneng Galaxy.

“Niliposoma CV (wasifu) wa huyu kocha mpya nimeamini kuwa viongozi wanapiga hatua kubwa kwa kuwa na jicho la kiufundi la kutambua timu inahitaji nini na malengo yake ni yapi,” alisema Rage, aliyewahi kuwa mwenyekiti wa Simba.

Aliongeza kuwa ujio wa kocha huyo una matumaini kuwa atafanya kile ambacho watangulizi wake walifanya hususan kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara.

“Viongozi wanapaswa wasimuingilie mipango yake hata kidogo. Wamsikilize kwanza ili waone makubwa yanayokuja, naamini lile pira biriani limerejea maana lilipotea kwa miaka ya hivi karibuni,” alisema.

Vilevile aliwataka mashabiki wa timu wasimpe presha akiamini kuwa kwa kufanya hivyo kutamfanya ashindwe kuwa na imani na anachofanya.

“Najua mashabiki wanahitaji mambo mazuri bila kujua mafanikio yanakuja taratibu. Hivyo wawe wastahimilivu ili waone matunda hapo baadae.”

Akizungumzia mchezo wa dabi ya Kariakoo utakaochezwa Desemba 11, Rage alisema Pablo hapaswi kupimwa kwa mechi hiyo ingawa anatambua kila shabiki wa Simba angependa kushinda kutokana na utani wa timu hizo pindi zinapokutana.

“Mafanikio yanapimwa kwa mataji na sio kufungwa. Najua Pablo anakuja katika kipindi ambacho mchezo huo unakaribia, lakini kikubwa ni kuchukua ubingwa mwisho wa msimu na sio vinginevyo.”

Naye kocha msaidizi wa kikosi hicho, Thierry Hitimana alisema ujio wa Pablo unatoa matumaini ya kikosi hicho kufanya vizuri kutokana na timu kubwa ambazo amezifundisha.

“Ni kocha mzuri ambaye naamini Simba wamepata mtu sahihi kutokana na aina ya ufundishaji wake na soka ambalo wanapenda kucheza. Kikubwa ni kwa viongozi kumwamini na kumpa ushirikiano,” alisema Hitimana.

Kabla ya kujiunga na Simba Pablo alikuwa anaifundisha Al Qadsia SC ya Quwait kuanzia 2019 hadi 2021. Mwaka 2015 alikuwa kocha mkuu wa Getafe CF inayoshiriki Ligi Kuu Hispania. Pia alikuwa kocha msaidizi wa Real Madrid 2018 chini ya Kocha Julen Lopetegui na baadaye Santiago Solari.

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz