Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Rage: Katiba Simba ibadilishwe

Vigogo Simba Kikaoni Katiba Simba ibadilishwe

Wed, 14 Dec 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Mwenyekiti wa zamani wa Klabu ya Simba, Ismail Aden Rage amewataka watakaochaguliwa kwenye Uchaguzi Mkuu wa klabu hiyo unaotarajiwa kufanyika Januari 19, mwakani, wapiganie mabadiliko ya katiba inayoonekana kutowapa uhuru viongozi waliochaguliwa na wanachama.

Akizungumza Rage alisema kwa upande wake haoni umuhimu wa uchaguzi huo kutokana na Katiba iliyopo kushindwa kuwabeba wanachama ambao ndio wana asilimia kubwa ya umiliki wa hisa.

“Wanachama wana asilimia 51, lakini hawana kauli kutokana na Katiba iliyopo kushindwa kuwapa nafasi ya kuzungumza jambo ambalo sio haki kwao,” alisema Rage.

“Endapo uchaguzi huo utafanikiwa kufanyika, basi viongozi watakaochaguliwa wafanye mchakato kuhakikisha wanabadili Katiba ili waweze kuwa na kauli kwa ajili ya klabu yao.” Rage aliwatakia wana Simba kila la heri kwenye mchakato wa uchaguzi na kwamba, anaamini kila atakayechaguliwa atafanyia kazi mabadiliko ya Katiba ili wanachama wawe na nguvu kulingana na asilimia zao.

Kwa mujibu wa Katiba, mwekezaji humiliki hisa asilimia 49 na ndiye mwenye mamlaka yote ndani ya klabu inayoongozwa na Bodi ya Wakurugenzi huku viongozi waliochaguliwa na wanachama wakiwa washirikishwaji.

Rage alisema wanachama ambao ndiyo wapiga kura wanatakiwa kuchagua viongozi waadilifu na sahihi katika kila jambo kwa maslahi ya klabu.

Chanzo: Mwanaspoti