Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

RIPOTI MAALUMU: Kituko cha mipira mitatu Ligi Kuu

EBE76E1C B97A 4DF0 BC60 6963766048E9.jpeg RIPOTI MAALUMU: Kituko cha mipira mitatu Ligi Kuu

Sun, 11 Dec 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Bodi ya Ligi Tanzania (TPLB), imekuwa ikiboresha vitu mbalimbali ili kupata michezo yenye ushindani bila ya kujali inachezwa kwenye viwanja gani au timu zipi zinazokutana wakati huo.

Miongoni mwa maboresho inayofanya uongozi wa bodi ni kuhakikisha viwanja vinavyotumika kwenye michezo ya ligi vinakuwa na ubora maeneo yote na hali nzuri ya kutumika pamoja na mambo mengine yote ya msingi. Bodi, licha ya kuhakikisha inasimamia maeneo yote kuwa kwenye ubora bado kuna eneo moja la msingi limekuwa na changamoto ambalo linatakiwa kufanyiwa kazi na kuboreshwa mapema.

Eneo hilo ni mipira ya kuchezea mechi kwa kila timu imekuwa changamoto kwenye klabu zilizopo Ligi Kuu Bara, hakuna mpira maalumu unaotumika kwenye michezo kila ukiangalia michezo mbalimbali ya ligi mipira inabadilika hakuna mmoja uliokuwa maalumu.

Kwenye ligi mbalimbali hata mashindano yaliyoendelea kuna mipira maalumu inayotumika kwenye mechi na hauwezi kukuta mipira tofauti ikitumika katika michezo ya mashindano au ligi hiyo iliyoendelea.

Kwa mfano mashindano yote ya ‘CAF’ ngazi ya klabu na timu za taifa mipira inayotakiwa kutumika ni Kampuni ya Umbro ikiwa ni moja ya kampuni kubwa zaidi ya vifaa vya michezo duniani.

Mipira hiyo inatakiwa kutumika siku moja kabla ya mchezo wa timu husika ikiwa kwenye mazoezi yanayofanyika uwanja wa mechi na mechi yenyewe.

Ushawahi kufikiria juu ya mpira wa soka wa kuchajiwa kama simu..? Basi kama unafuatilia fainali za Kombe la Dunia 2022 za huko Qatar, mipira inayotumika yote inachajiwa kwa umeme kama simu tu.

Mipira inayotumika kwenye fainali za Kombe la Dunia 2022 imetengenezwa kwa teknolojia kubwa sana, ikiwekewa ‘chip’ maalumu ndani, zinahitaji kuwa na nishati ya umeme kufanya kazi kwa usahihi.

Mipira ya soka inayotumika huko Qatar ikiwa inachajiwa, imewaacha kwenye mshangao mkubwa mashabiki wengine wakidai kweli duniani kuna mambo.

Mipira ya Kombe la Dunia 2022, iliyotengenezwa na Kampuni ya Vifaa vya Michezo ya Adidas ina sensa ndani yake, ambayo inakusanya takwimu mbalimbali, kasi na uelekeo wa mpira na kutuma ujumbe kwenye mashine za VAR kutambua kama kuna mchezaji ameotea (offside) na hata mpira ukitoka nje au la.

Nikukumbushe tena kombe la dunia mwaka 2010, Afrika Kusini mipira iliyotumika, Jabulani, ilitengenezwa na Kampuni ya Adidas ilijizoelea umaarufu mkubwa ila baadhi ya wachezaji walikuwa wakiilalamikia huku Mshambuliaji wa Uruguay, Diego Forlan akiisifu kwani aliweza kuitumia vyema ikiwemo kufunga mabao ya aina mbalimbali. Turudi kwenye ligi yetu sasa;

LIGI YETU MIPIRA GANI INATUMIKA?

Kwenye Ligi Kuu Bara hadi sasa hakuna mpira maalumu kama katika mashindano au ligi mbalimbali zilizoendelea kama zilizoonyeshwa mwanzo wa makala haya.

Miaka ya nyuma mdhamini wa ligi (Vodacom), alikuwa akitoa vifaa mbalimbali kwa timu zote ikiwemo, viatu, jezi, mabegi, mipira pamoja na mambo mengine ya msingi.

Kwahiyo wakati huu hakuna mpira maalumu unaotumika kwenye ligi kwani Bodi ya Ligi hutoa mitano tu kwa kila kituo ambayo kwa msimu mzima huwa haitoshi kutumika kwenye mashindano yote hata kwenye Ligi Kuu Bara.

Jambo hilo linachangia baadhi ya timu kununua mipira yake yenyewe kwa ajili ya mechi pamoja na kufanyia mazoezi.

Meneja wa Namungo, Idrissa Bandari ameliambia Mwanaspoti kuwa kwenye kila kituo kwa maana chama cha soka mkoa kunakuwa na mipira mitano waliyopewa na Bodi ya Ligi, ili kutumika kwenye ligi zote zilizopo kwenye mkoa husika.

“Ila nadhani mipira hiyo mitano hutumika kwenye michezo ya Ligi Kuu Bara tu huko kwenye mashindano mengine hutumika mipira tofauti na hii iliyotoa Bodi,” anasema Bandari na kuongeza;

“Wakati tunakwenda kucheza na Geita Gold kulikuwa hakuna mipira wa bodi ilikuwa bado haijafika huko kwahiyo timu yetu ilitoa mitano na wapinzani walitoa mitano tukatumia kwenye mechi yetu ambayo siyo ile inayotakiwa kutumika kwenye ligi,”

“Simba na Yanga nahisi wamenunua mipira inayofanana na ile mitano ya bodi, pengine huwa wanatumia katika michezo yao ndio maana kuna nyakati mchezo mmoja huonekana mipira miwili tofauti.

“Kabla ya mdhamini kubadilika tulikuwa tunapewa vifaa mbalimbali ikiwemo mipira ila sasa hivi hilo hakuna.”

MIPIRA GANI ILIYOTOLEWA?

Mipira mitano iliyotolewa na bodi ni Uhlsport inatajwa kwenye listi ya mipira bora ambayo imekuwa ikitumika kwenye ligi mbalimbali kubwa duniani ikiwemo Tanzania.

Mipira hii ina viwango vyote vinavyotakiwa, ikiwa na ukubwa sahihi unaruhusiwa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), ikiwa inazalishwa na Kampuni ya Uhlsport ilianzishwa mwaka 1948, nchini Ujerumani.

Lakini sasa kilichotokea kutokana na ishu ya gharama kwenye mechi tofauti za Ligi Kuu kumekuwa kukionekana mipira mitatu yenye rangi tofauti. Mmoja ule halisi na mingine ya kuchakachua.

BEI ZA MIPIRA HIYO MITATU?

Miongoni mwa sababu inayochangia baadhi ya mechi za ligi kutumika mipira tofauti na ile ya Uhlsport ni gharama kwani mmoja ule orijino kabisa unauzwa Sh200,000 kwahiyo siyo timu zote zinazoweza kununua.

Timu chache kama Yanga, Azam, Simba na nyingine zinaweza kununua mipira hiyo ikawa nayo mingi tofauti na timu nyingine hadi kutumia kwenye michezo yao inapokuwa Uwanja wa Benjamin Mkapa na vile vya mikoani.

KWA NINI KWENYE LIGI MIPIRA TOFAUTI?

Huenda kuna baadhi ya wapenzi na wadau mbalimbali wa soka wanagundua na wasiogundua kuwa kwenye michezo mbalimbali ya Ligi Kuu Bara mipira inayotumika haifanani rangi wala kiwango cha ubora (angalia pichani).

Kwa mfano, ukiangalia mechi ya Kagera Sugar dhidi ya Tanzania Prisons kuna baadhi ya mipira itakuwa tofauti na mchezo wa Ruvu Shooting dhidi ya Namungo si kwa michezo hiyo tu, bali hata ile ya Azam, Simba na Yanga.

Miongoni mwa sababu ni Wadhamini wa Ligi (NBC), hawatoi mipira kwa timu, bodi inatoa mipira mitano kwa kila kituo ambayo haitoshi na timu klabu nyingine zenye uwezo zinajinunulia mipira yenyewe na kama ikitaka kama ile ya ligi mmoja si chini ya Sh200,000.

Si rahisi kila timu kununua mipira inayofanana na ile ya ligi ndiyo maana kumekuwa na changamoto hiyo.

WAFUNGA HAT-TRICK VITUKO TUPU

Msimu uliopita kwenye Ligi Kuu Bara wachezaji watatu walifunga mabao matatu kwenye mchezo mmoja (hat-trick), Idrissa Mbombo wa Azam, Shiza Kichuya wa Namungo na Jeremia Juma wa Tanzania Prisons.

Msimu huu hadi mzunguko wa kwanza unamalizika wachezaji wawili wamefunga hat-trick, Fiston Mayele wa Yanga na nahodha wa Simba, John Bocco ambao taarifa zinaeleza hakuna aliyepewa mipira baada ya mechi pamoja na kwamba kwenye kamera wamekuwa wakionekana wakikabidhiwa.

Mayele aliyefunga hat-trick mchezo wa Singida Big Stars na Bocco aliyefunga hat-trick dhidi ya Ruvu Shooting wote baada ya mechi kumalizika walionekana kupewa mipira na waamuzi ikiwemo kupiga nayo picha na kabla ya kuingia kwenye vyumba vya kubadilishia nguo walionekana wakirudisha mipira hiyo kwa waamuzi tofauti na ilivyokuwa ikifikiriwa na wengi kuwa wataondoka nayo kwenda kuweka kumbukumbu. Mara nyingi wamekuwa wakiambiwa kuwa kuna mingine tofauti na hiyo watapewa.

Sababu zilizofanya wachezaji hao kutopewa mipira kwanza kwenye kituo ipo michache (mitano) na nyingine hiyo mipira inayotumika kwenye michezo yao si ya bodi bali ya timu zao kwahiyo wakiichukua maana yake klabu husika inapungukiwa na idadi ya mipira iliyonunua yenyewe.

Jeremia, anasema msimu uliopita baada ya kufunga hat-trick kwenye mechi ya Namungo waamuzi walitaka kumpokonya mpira na wakamueleza atapewa siku nyingine na uongozi wa TPLB ila mwenyewe aligoma na kuutaka uleule.

“Nakumbuka niligoma kabisa na wala sikutaka maelezo yao nilikuwa nataka mipira uleule niliyotumia kufunga baada ya mchezo kumalizika nilipewa na sikurudisha tena kama waamuzi walivyokuwa wanahitaji,” anasema Jeremia na kuongeza;

“Baada ya Bocco kufunga hat-trick mechi na Ruvu msimu huu akiwa anaelekea vyumba vya kubadilishia nguo alirudisha mpira kwa waamuzi, jambo ambalo halikuwa sahihi kwani naamini alipewa mipira siku nyingine na ulikuwa tofauti na ule uliotumika kwenye mechi husika.”

BODI YA LIGI

Mkurugenzi wa Bodi ya Ligi (TPLB), Almas Kasongo anasema mpira unaotumika kwenye mechi zote za Ligi Kuu Bara ni mmoja na wasimamizi wa vituo vyote wanafahamu hilo na hakuna utofauti wowote.

Kasongo anasema kama kuna utofauti wowote kwenye mipira inayochezwa michezo wa Ligi Kuu Bara hadi mzunguko wa kwanza unamalizika halifahamu hilo. “Sijakutana na kesi ya aina hiyo na viongozi wote wanajua mpira unaopaswa kutumika ni mmoja kwenye Ligi Kuu Bara na huo ndio utaratibu,” anasema Kasongo na kuongeza;

“Suala la mipira kutokuwapo kwenye (FA) za Mikoa ni changamoto za kikanuni ila wanapaswa kuwa nayo ingawa inatakiwa kutimiza kanuni kuwa na mipira ya kutosha.”

Anasema matatizo mengine ni kwa wachezaji kutokuwa na elimu ya kutosha na kutofuatilia na kuuliza huku akikiri kuwa zipo baadhi ya changamoto kwenye mamlaka akifafanua kuwa wanaendelea kuzifanyia kazi.

VYAMA VYA MIKOA

Kaimu Mwenyekiti wa Chama cha soka mkoani Mbeya, (MREFA), Sadick Jumbe anasema kwenye kanuni hakuna ilipoandikwa mchezaji wa daraja la nne, la tatu, First league wala championship kuwa atakabidhiwa mpira akifunga Hat-trick.

“Chama cha soka hakina mipira ya kutoa kwani inapotokea mchezaji akafunga kwenye uwanja wowote mkoani humo, MREFA itawasiliana na bodi ili kupata haki yake,” anasema Jumbe na kuongeza;

“Sisi mipira hatuna, iliyopo inatoka bodi kwa ajili ya Ligi Kuu Bara, kanuni za Mrefa Ligi za Wilaya na Mkoa hakuna wanatumia mipira yao, msimu ujao tunaenda kulijadili hili kwenye kikao nakuahidi litatekelezeka,” anasema Jumbe.

SIMBA, YANGA ZAINGIA HASARA

Inaelezwa Simba na Yanga zimeingia hasara msimu huu kwani kabla ya kuanza zilinunua mipira ya Uhlsport yenye rangi ya bluu na kijivu ikiamini inakwenda kutumika kwenye ligi.

Ukiangalia mechi ya Ngao ya Jamii mipira iliyotumika ilitolewa na Simba (Uhlsport), dhidi ya wapinzani wao Yanga ila msimu ulipoanza TPLB ilitoa mipira ya kampuni hiyo lakini rangi tofauti na ile waliyonunua awali.

Mmoja wa watalaamu kutoka Simba anasema mipira inayotumika kwenye ligi msimu huu hawana kwani kabla ya kuanza walinunua ile ya Uhlsport iliyokuwa na rangi ya bluu na kijivu.

“Msimu ulipoanza ilitoa mipira yenye rangi nyingine Uhlsport yenye rangi ya kijani na kijivu jambo ambalo lilikuwa tofauti na makubaliano ya awali kwahiyo Simba hatuna hiyo,” anasema mtaalamu huyo.

MAKIPA WA LIGI

Kipa wa Singida Big Stars, Aboubakar Khomein, anasema kuna baadhi ya mipira imekuwa na changamoto kwenye uwanja wenye upepo inakuwa hautulii kama ikiwa katika uwanja usiokuwa na eneo zuri la kuchezea.

“Ukiangalia hata bao nililofungwa na Simba ilitokana na mipira kubadilika uelekeo kwani mfungaji wa bao, Peter Banda hakupiga kwa kulenga goli,” anasema Khomein.

Chanzo: Mwanaspoti