Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

RIPOTI MAALUM: Haya ndiyo wanayopitia waamuzi wa soka wanawake

Tatu Malogo CAF RIPOTI MAALUM: Haya ndiyo wanayopitia waamuzi wa soka wanawake

Wed, 15 Nov 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Wakati soka la wanawake linazidi kukua kutokana na kuongezeka kwa timu za jinsi hiyo kila uchao, bado kuna idadi ndogo ya waamuzi wa soka wa kike Tanzania.

Kwa sasa Tanzania kuna Ligi Kuu ya Wanawake (WPL), Ligi za Mabingwa wa Mikoa kwa Soka la Wanawake mbali na Daraja la Kwanza (WFDL) ambazo kimsingi mechi zake zinapaswa kuchezeshwa na waamuzi wa kike.

Ongezeko la timu za soka za wanawake linatoa ulazima wa kuwapo kwa waamuzi wa kike wa kutosha ili kuwa na wahusika wenyewe wa jinsi hiyo..

Tatizo lililopo ni waamuzi kuwa wachache kitu ambacho kinaibua maswali mengi ni kitu gani hasa kinachokwamisha.

Kama soka la wanawake mwamko umekuwa mkubwa, kwanini waamuzi hawahamasiki kuongezeka?

Hapa Tanzania Bara kwa ujumla kuna waamuzi 800 kwa ligi zote za soka, lakini wanaochezesha Ligi Kuu Bara ni 70, waamuzi wa kati wapo 30 na wasaidizi ni 40.

Ligi ya Championship kuna waamuzi 96, waamuzi wa kati wako 32 na wasaidizi ni 64, First League wapo 136 wa kati wakiwa ni 64 na wasaidizi 72.

Pia kuna waamuzi 220 ambao huchezesha ligi nyingine zilizopo chini ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kama Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC), Ligi ya Mabingwa wa Mkoa (RCL), U-20, U-17, Wilaya na Ligi ya Wanawake.

Ukiangalia nchi kama Kenya inakadiriwa kuwa na waamuzi 10,000 kwenye ligi zote, huku kwenye Ligi Kuu ina waamuzi 94 na kati ya hao 25 ni wanawake.

Kati ya wanawake hao, watano wana beji ya FIFA, watatu ni waamuzi wasaidizi na wawili ni waamuzi wa kati, na inadaiwa kwamba waamuzi wa kike walianza kujiunga na kazi hiyo mwaka 1980 sawa na Tanzania ambayo mwamuzi mstaafu Elizabeth Kalinga alikuwa ndiye mwamuzi wa kwanza wa kike nchini.

Kwa waamuzi wote hao, Kenya wamegawanyika katika ligi tofauti hadi za madaraja tofauti ya chini.

TATIZO NI NINI?

Kwenye fainali za Kombe la Dunia la Soka la Wanawake (Women’s World Cup 2023) zilizofanyika mwaka huu huko Australia, karibu mechi zote zilichezeshwa na waamuzi wa kike - hiyo inafanya umuhimu wao kuongezeka kwenye mchezo huo duniani.

Waamuzi wanawake wamekuwa wakipewa pia nafasi za kuchezesha mechi za soka za wanaume na hiyo imekuwa ikifanyika hata kwenye mashindano makubwa kama ya Kombe la Dunia la Fifa na Ligi Kuu England, michuano yenye ushindani mkubwa zaidi, lakini waamuzi wa kike wamekuwa wakipewa dhamana ya kuchezesha mechi hizo.

Hilo linafungua njia kwa Tanzania kuongeza nguvu kwenye kuandaa waamuzi wa soka wa kike wa kutosha, kwa sababu anapochaguliwa kwenda kuchezesha mechi za michuano mikubwa nje ya nchi ni sehemu ya kuitangaza kimataifa.

Hapa Tanzania wapo waamuzi wa soka wanawake wanaopewa nafasi ya kucheza mechi kubwa kama za Simba na Yanga, ambao mfano wake ni Jonesia Rukyaa na Tatu Malogo.

Kuna waamuzi wachache pia wa kike wenye beji ya FIFA, ambao wanafuzu kuchezesha mechi za kimataifa, huku Rais wa Shirikisho la Kimataifa la Vyama vya soka (Fifa), Gianni Infantino anasema ni wakati sahihi wa wanawake kupewa nguvu kubwa katika ushiriki wao wa mchezo wa soka, huku mpango ukiwa ni kuongeza timu zitakazoshiriki mashindano ya Kombe la Dunia na Fifa inalenga kuwekeza Dola 1 bilioni kwenye soka la wanawake.

Hiyo ni fursa kubwa inayopaswa kuchangamkiwa na Tanzania kama taifa linalokuwa kwa kasi kwenye soka la wanawake baada ya timu yake ya vijana ya chini ya umri wa miaka 18, kuwahi kushiriki fainali za Kombe la Dunia kwa timu za vijana na kufika hatua ya robo fainali.

Kama kwenye anga ya kimataifa, mtazamo uliopo ni kulipa soka la wanawake nafasi kubwa, kwanini Tanzania kuna kundi dogo la wanawake wanaojiingiza kwenye kazi ya uamuzi?

Uchache wao umesababisha hata Ligi Kuu ya Wanawake na Ligi ya Mkoa ya Wanawake kuchezeshwa na waamuzi wa kiume, wakati ilipaswa kuwa eneo la waamuzi wa kike kuonyesha umahiri wao.

Katika makala haya maalumu, tunaangazia mambo mbalimbali kujua nini kinakwamisha, je, hawapewi nafasi? Ugumu uko wapi kwenye kozi za uamuzi, kuna rushwa? Wananyanyaswa? Chama cha Waamuzi (FRAT) kinachukua hatua gani? Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara wanasemaje? Jamii inaweza kuwa kikwazo kwao kujihusisha na uamuzi?

Je, familia inaweza kuwa kikwazo kwao? Kuna madai kwamba waamuzi wa kike wanapungua kwa sababu wale ambao wapo kwenye familia wanapofanikiwa kupata watoto tu, inakuwa shida kuendelea na kazi hiyo.

Uamuzi unawanyima fursa ya kuzaa au kuolewa kwasababu hiyo itashusha viwango vyao vya uchezeshaji, kuna ukweli juu ya hilo? Na kuna ugumu kwa mwamuzi kutimiza majukumu yake ya uamuzi wakati akiwa mzazi?

FRAT ambao ndiyo hutengeneza waamuzi nchini na kuwakabidhi kwenye Kamati ya Waamuzi iliyo chini ya TFF na ambayo inatambulika na FIFA, inafafanua ni kwanini kuna idadi ndogo ya waamuzi wa kike ukilinganisha na wanaume.

Katibu Mkuu wa FRAT, Kennedy Mapunda anasema; “Malengo ni kuwa na waamuzi bora na sio idadi kubwa ya waamuzi, ingawa changamoto ipo kwa watoto wa kike kujiingiza kwenye fani hii.

“Mwitikio kwa wanawake ni mdogo kwasababu imejengeka imani kwamba huu mchezo ni wa kiume, wengi wanaogopa kutukanwa, kupigwa na hata kudhalilishwa, hivyo jamii haikubaliani moja kwa moja wanawake kuingia huku.

“Kufikisha 50/50 hapa kwetu ni vigumu, kwanza mwanamke hata akiwa kwenye fani hii ni vigumu kudumu kwa miaka mingi kwani atahitaji awe na familia yake, hivyo akiingia huko lazima kuna kupata watoto na wengi wao wakishaingia kwenye mambo ya uzazi si rahisi kumudu.

“Sisi kama FRAT kazi yetu ni kupika waamuzi tu na kuwakabidhi kwenye kamati ambayo inatambulika FIFA kwa mujibu wa taratibu zao, maana FIFA anayetambulika ni Kamati na sio FRAT ndiyo maana mwamuzi akiadhibiwa anapelekwa kwenye kamati na sio kwetu,” anasema Mapunda.

IDADI YA WAAMUZI

Mkufunzi wa Waamuzi kutoka CAF ambaye ni Mtanzania, Leslie Liunda anasema hadi sasa kwa Tanzania waamuzi wenye beji ya Fifa wako 13, wanne kati ya hao ni wanawake ingawa hadi sasa ni mmoja tu Tatu Malogo ndiye mwenye beji ya FIFA na anapangiwa mechi za kimataifa wakati wasaidizi ni watatu Janeth Balama, Glory Tesha na Zawadi Yusuph.

Awali, alikuwepo Florentina na Jonesia Rukyaa. Florentina hataweza tena kuomba beji hiyo wakati Jonesia ana nafasi ya kuomba baada ya kufeli kozi ya kwanza.

Wanaume wapo tisa, wanne ni waamuzi wa kati ambao ni Elly Sasii, Ramadhan Kayoko, Ahmed Arajiga na Nasri kutoka Zanzibar, wasaidizi wapo watano Frank Komba, Mohammed Mkono, Ally Ramadhan (Zenji), Hamdan Said, Kassim Mpanga huku Sudi Lila akiwa na kazi ya kuisaka tena kama ilivyo kwa Jonesia.

“Nchi nyingi zipo hivyo, waamuzi wa kati ni wachache kuliko wasaidizi, kila mchezo unahitaji refa mmoja na wasaidizi wawili na anayekaa mezani.

“Ili kutengeneza timu yenye uwiano mzuri lazima namba ya waamuzi wasaidizi iwe kubwa, nchi nyingine zina waamuzi watano ama sita ingawa kwa asilimia 70 wanakuwa wanne,” anasema Liunda

“Kupata beji ya FIFA kwanza uwe na kiwango kizuri mfululizo pia angalau utumikie ligi ya nyumbani kwa miaka miwili kwa kiwango kile kile, uchezeshaji wake, mitihani na majaribio anayofanya iwe kwa viwango vya juu, hivyo tathmini inafanyika kwa ujumla.

“Majina yanajumuishwa na kupelekwa FIFA na yakipelekwa sio lazima yakubalike yote, kuna kukubaliwa ama kukataliwa hata kama una sifa zote.

“Kuna ugumu kidogo maana mwanamke sasa analazimika kufanya kitu ambacho kinatumia nguvu ambayo kwa wanaume ni kitu rahisi, mwanamke analazimika kwenda kwenye viwango vya wanaume kitu ambacho si rahisi.

“Baada ya kubaki na jina moja la mwamuzi wa kike, tumepeleka jingine Amina Kyando aliyefanya vizuri ile kozi ya Agosti hivyo majina yalienda mawili pamoja na la Tatu. Tuna uhakika jina la Tatu litarudi ila Amina hatuna uhakika kama Junuari watampa beji maana ni uamuzi wao ila tunaomba watupe.

“Akiwa mwamuzi mwenye beji ni mmoja tu, inamnyima fursa kupata nafasi FIFA kwasababu wanapokwenda kuchezesha mechi wanatakiwa wawe waamuzi wawili na wasaidizi wawili kutoka nchi moja, sasa akiwa mmoja basi mwingine analazimika kutoka nchi nyingine.

“Upande wa wanaume sio shida sana, wapo wanne na tumeomba wawe watano hivyo tunasubiri, Ester alikuwa miongoni mwa waamuzi wa kati ambao tungepeleka majina yao ila ilishindikana kwasababu alikuwa anaumwa hivyo hakufanya vizuri kwenye mitihani,” anasema Liunda.

MAZOEZI YAO

Liunda anasema kuwa: “Mafunzo ya darasani hakuna tofauti kati ya wanawake na wanaume, kwasababu wote wanaenda kuchezesha mpira wenye sheria 17, lakini katika utimamu wa mwili ndipo pana utofauti kidogo.

“Kama kuna wasichana ambao watashiriki kuchezesha michezo ya wanaume kama Ligi Kuu, Championship, First League wanapaswa kukimbia katika viwango vile ambavyo waamuzi wa kiume wanakimbia ila tofauti ni muda.

“Wanawake muda unapungua kidogo, ili kuona ile kasi haiwi na tofauti kubwa. Wanapokuwa wanakimbia, wanaume wanatakiwa kukimbia kwanza, kunakuwa na mbio fupi za mita 10 ndani ya sekunde sita na wanawake sekundi 6.40. Ni lazima wafanye hivyo kama wanawake watashiriki ligi ya wanaume basi ni lazima wakimbie mita 40 ndani ya sekunde sita.

“Pili kuna mbio ndefu wanakimbia mita 75 halafu wanatembea kisha wanakuja kumalizia kukimbia tena mita kama hizo kuzunguka ule uwanja ili kutengeneza raundi moja, na ili afaulu anatakiwa akimbie raundi 10 ambayo jumla yake inakuwa mita 3000 chini ya hapo anakuwa amefeli, hii ni kwa ngazi zote kuanzia ligi ya ndani hata kimataifa na Kombe la Dunia.

“Ila kwa yeyote anayeonekana anachezesha ujue amefaulu zile mbio fupi kwamaana amekimbia kwa muda unaotakiwa, mwenye beji ya FIFA hatolewi kwasababu ile ya FIFA inafanyika mara moja kwa mwaka na baada ya pale kila baada ya miezi mitatu unakimbia tena hivyo kwa mwaka wanakimbia mara nne.

“Kuomba beji ya FIFA kozi hufanyika Julai kwenda Agosti, na mwaka huu imefanyika, hizi kozi zinazofanyika Septemba, Desemba, Januari na Machi ni za kujiweka fiti na kama umefeli unapaswa kurudia kati ya miezi hiyo.

Chanzo: Mwanaspoti