Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Amos Makalla, ameahidi kuweka mikakati madhubuti yenye lengo la kuboresha na kuinua mchezo wa mpira wa miguu mkoani humo ambao umeonekana kudolola kwa kipindi kirefu sasa.
Makala ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na watumishi pamoja na viongozi wa idara mbalimbali na kusema kuwa pamoja na mambo mengine atahakikisha anaweka uhamasishaji na kuwafanya mashabiki kuwa wazalendo na timu za ndani ya mkoa huo.
“Nitahakikisha napandisha timu ligi kuu katika msimu unaokuja maana ni aibu Mkoa wenye rasilimali kubwa za kiuchumi, jiographia nzuri ya kiutalii, watu wengi haiwezi kukosa timu ligi kuu hii itasababisha tunakosa mapato hususani pale ambapo timu mbalimbali zitahitajika kufika mkoani hapa na kuchangamsha Jiji.
Ameongeza kuwa "Tukishakuwa na timu ya Ligi Kuu basi makundi yote na wafanyabiashara watakuja hapa na kukuza uchumi wa mkoa wetu na kuchochea ukuaji wa sekta mbalimbali,”
Kwa sasa mkoa huo hauna timu inayoshiriki Ligi Kuu, ukiwa na timu mbili za Championship (Pamba na Copco) na Mapinduzi ikiwa First League (daraja la pili), huku Mbao, Toto Africans na Gwambina zikiwa ngazi ya mkoa.