Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Pumzi imekata, Varane anapokimbilia mwisho wa soka lake

Varane Azima Tetesi Za Kuhamia Saudia Rafael Varane

Thu, 16 Nov 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Kocha wa Manchester United, Erik ten Hag alilazimika kumtema katika kikosi cha kwanza Raphael Varane ambaye msimu uliopita alikuwa na mchango mkubwa sana.

Beki huyo wa zamani wa kimataifa wa Ufaransa wakati anatua Old Trafford alisema: “Man United ni moja ya klabu maarufu duniani na kupata nafasi ya kuja kukipiga hapa ni kitu ambacho nisingeweza kukataa. Ninataka kuisaidia timu kushinda kila kitu ili kutengeneza historia ndani ya klabu hii.”

Varane alionekana kuwa beki sahihi wakati anajiunga mwaka 2021 ambaye angesaidia kuhamasisha timu ili kupata mataji kwani ana uzoefu mkubwa na Man United ingenufaika na uwepo wake kutokana na mafanikio mengi aliyopata wakati anakipiga Real Madrid.

Klabu hiyo iliwekeza Pauni 40 milioni kuinasa saini yake mwaka 2021 alipokuwa na umri wa miaka 28 baada ya uamuzi wake wa kuondoka Madrid na ilionekana kama biashara ya busara wakati huo.

Baada ya kucheza misimu 10 Los Blancos na kufikisha mechi 360, mataji manne ya Ligi ya Mabingwa na mataji matatu ya La Liga, Varane aliondoka Santiago Bernabeu kama nguli wa klabu hiyo.

Lakini Madrid iliendeleza ubabe na kubeba mataji mawili -- Ligi ya Mabingwa Ulaya na Ligi Kuu Hispania -- katika msimu wao wa kwanza bila Varane, ambaye lazima atakuwa amejutia uamuzi wake wa kuondoka kufuatia msimu mbaya akiwa na uzi wa Man United.

Kitendo cha Ten Hag kumchagua Varane katika kikosi cha kwanza msimu wa 2022-23 kiliamsha ubora wake baada ya kuanza kwa kusuasua akicheza sambamba na beki wa kimataifa wa Argentina, Lisandro Martinez, wawili hao walikuwa mhimili muhimu kwenye safu ya ulinzi na walikuwa chachu ya ushindi wa Man United na hatimaye wakabeba Kombe la Carabao baada ya kuifunga Newcastle mabao mawili katika mechi ya fainali iliyochezwa kwenye Uwanja wa Wembley.

Msingi huo thabiti kwenye safu ya ulinzi ulikuwa muhimu kwani Mashetani Wekundu walirejea katika michuano ya Ligi ya Mabingwa baada ya kumaliza msimu wakiwa nafasi ya tatu msimu uliopita.

Licha ya kufikisha umri wa miaka 30, bado alionyesha kiwango kizuri na alistahili kuwepo kwenye kikosi cha kwanza cha kudumu cha Ten Hag, lakini katika muda wa miezi michache tu mambo yakabadilika na kumwendea hovyo kabisa.

Bingwa huyo wa Kombe la Dunia ghafla ameanza kusugua benchi na kuwa chaguo la nne katika mpangilio wa nafasi ya beki wa kati wa Man United, pia hajumuishwi kikosini mbele ya beki Jonny Evans.

Evans mwenye umri wa miaka 35 alijiunga tena na klabu hiyo kwa uhamisho wa kushtukiza bila malipo kwenye usajili wa dirisha la kiangazi lililopita.

Man United sasa inaonekana safu ya ulinzi imetulia bila ya Varane, ni vigumu kuona namna yoyote ya kurejea kwake. Nini sababu ya anguko la beki huyo kisiki wa zamani wa Madrid kwa sasa?

KUREJEA KWA MAGUIRE

Beki huyo alipondwa sana wakati fulani kutokana na kiwango chake mpaka inafikia mashabiki wanamzomea uwanjani. Maguire alivumilia kipindi kigumu na kuvuliwa kitambaa cha unahodha ambacho alikabidhiwa kiungo Bruno Fernandes. Aidha licha ya kupitia kipindi kigumu beki huyo amerejea kwa kishindo na amekuwa na mchango mkubwa timu yake, hivi karibuni alikuwa shujaa alipoifungia bao timu yake kwenye mechi muhimu ya Ligi Mabingwa Ulaya dhidi ya Copenhagen, Pia alikuwa shujaa kwenye mechi ya Ligi Kuu England dhidi ya Sheffield akiisaidia timu yake kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 mwezi uliopita. Kutokana na kiwango bora cha Maguire, haikuwa shida kwa Ten Hag kufanya uamuzi mgumu na kuanza kumuamini upya beki huyo.

PUMZI IMEKATA

Hata kabla ya Varane kuondolewa kwenye kikosi cha Ten Hag katika mechi ya kwanza ya Man United msimu huu dhidi ya Manchester City, kulikuwa na dalili za kiwango chake kushuka. “United ina udhaifu fulani,” kocha msaidizi wa zamani wa klabu hiyo Rene Meulensteen alisema katika mahojiano na kituo cha televisheni cha ESPN. “Varane hawezi kumudu kasi. Ligi Kuu England ina nguvu. Kila kitu kinakwenda kwa kilomita 100 kwa saa.”

Varane amepoteza kasi ambayo ilimfanya kuwa mgumu sana kumpita kule Real jambo ambalo limewaruhusu washambuliaji wa upinzani kumfunga tela kwa urahisi sana.

PRESHA YA KUSTAAFU KIMATAIFA

Varane alionyesha kwa mara ya kwanza kukatishwa tamaa kwenye fainali za Kombe la Dunia mwaka jana huko Qatar, ambapo Ufaransa ilitinga fainali ya pili mfululizo na kulala dhidi ya Argentina, iliyoongozwa na Lionel Messi kwa mikwaju ya penalti. Nyota huyo wa United alicheza mechi yake ya 93 katika mpambano huo lakini baadaye akatangaza kustaafu soka la kimataifa, jambo ambalo lilimkasirisha kocha wa Ufaransa, Didier Deschamps. Pengine Varane alifanya uamuzi wa mapema ya kustaafu soka la kimataifa.

Chanzo: Mwanaspoti