Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Promota pambano la Mwakinyo afungiwa

Promota Mwakinyoooooo Mangungu, Mo Dewji uso kwa macho Simba

Thu, 13 Jun 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Wakati wapenzi na mashabiki wa Simba wakikomaa wakimtaka, Mwenyekiti wa klabu hiyo, Murtaza Mangungu kuachia ngazi kama ilivyotokea kwa wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi akiwamo aliyekuwa Mwenyekiti, Salim Abdallah ‘Try Again, mwenyewe amevunja ukimya akisema hajiuzulu ng’o.

Mangungu amesema wanasubiri uteuzi wa wajumbe wa bodi ya wakurugenzi wa upande wa mwekezaji ndipo wachague mwenyekiti wa Bodi.

Amesema mpaka sasa hakuna mjumbe wa bodi ya wakurugenzi waliochaguliwa na wanachama ambaye amejizulu nafasi yake na hawaoni sababu ya kufanya hivyo kwa haraka.

Hatua ya Mangungu kusema hayo imetokana na kauli ya aliyekuwa mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi kutoka upande wa mwekezaji, Salim “Try Again” Abdallah kujiuzulu nafasi yake.

“Ni kweli kwa sasa hakuna mwenyekiti wa bodi wa klabu na hawezi kumshauri Try Again na wajumbe wengine wa upande wa mwekezaji kubadili maamuzi yao. Hayo ni maamuzi binafsi ambayo yametokana na mtazamo binafsi pia.

“Kwa sasa ni kusubiri upande wa mwekezaji kuchagua wajumbe wengine kwa mujibu wa taratibu na mwenyekiti atatokana na kura zitakazopigwa,” alisema Mangungu ambaye mashabiki wa Simba wamekuwa wakimrushia lawama kila timu inapoyumba kuliko upande wa muwekezaji.

Alifafanua kuwa suala la mwenyekiti wa bodi ni mchakato na hauwezi kwenda kwa kuteuana tu. “Tuna taratibu zetu ambazo zipo kwa mujibu wa taratibu, lengo hapa ni kuwa na uongozi ambao unafuata taratibu hizo, hivyo tunaomba mtusaidie kuhusiana na hili, kwani si la Mangungu, ni la taratibu.”

Aliongeza kuwa uongozi wa klabu bado upo imara pamoja na haya yanayoendelea kutokea kutoka kwa baadhi ya wanachama na mashabiki.

“Kwa upande wa viongozi wa klabu ambao wapo chini yangu, bado tupo madarakani na hii inatokana na dhamana tuliyopewa na wanachama, hakuna aliyejizulu mpaka sasa kwani sina barua yao. Wao na mimi tutaendelea kuiongoza klabu kwa mujibu wa taratibu zilizopo.

Pia lazima ijulikane kuwa, kila mtu au kiongozi ana maamuzi yake. Hivyo ikitokea kiongozi amejiuzulu, basi nitaheshimu maamuzi yake, kwani itakuwa kwa mujibu wa taratibu,” alisema Mangungu. Mpaka tunakwenda mitamboni jana usiku hakukuwa na mjumbe aliyekuwa amejiuzulu.

Lakini kuna mambo 10 ambayo Mo Dewji kama atapitishwa kwenye nafasi hiyo ya Mwenyekiti atakumbana nayo atakapoanza kazi Simba;

USAJILI

Kilio kikubwa cha Wanasimba ni sehemu ya usajili wa kikosi chao ambapo inatajwa kwamba ndiyo imewafelisha zaidi kipindi hiki ambacho wanajitafuta kurudi kwenye njia yao ya utawala. Msimu uliomalizika, Simba imeshika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi, kitu ambacho kimewaumiza zaidi Wanasimba kwani msimu ujao wanakwenda kushiriki Kombe la Shirikisho Afrika na siyo Ligi ya Mabingwa.

Wengi walioingia kikosini hapo wameshindwa kutoa matokeo chanya akiwemo Aubin Kramo ambaye msimu mzima alikuwa majeruhi, Pa Omar Jobe na Babacar Sarr walioingia dirisha dogo wameshindwa kukata kiu ya mashabiki. Wapo waliofanya vizuri akiwemo Ayoub Lakred na Freddy Michael licha ya kuanza taratibu.

Hao ni kwa upande wa wachezaji wa kimataifa ambao ndiyo wanatolewa macho zaidi na Wanasimba kwani wanaamini kutokana na kushiriki kwao michuano ya kimataifa basi wanapaswa kusajili majembe ya maana kutoka nje na siyo kujaza wasiokuwa na faida.

Mo Dewji ana jukumu kubwa la kuhakikisha Simba inafanya usajili mzuri na wenye tija kwa timu jambo ambalo litarudisha ushindani wao katika michuano wanayokwenda kushiriki. Kumbuka kwamba tunaelekea kipindi cha usajili wa dirisha kubwa.

Kuhusu usajili, Mo Dewji amesema: “Tumekuwa tukisajili wachezaji wengi ambao wameshindwa kukidhi kiu ya Wanasimba, nataka niwaambie Wanasimba tutakwenda kufanya usajili mzuri utakaorudisha ubora wa kikosi chetu.”

SAFU YA UONGOZI

Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba upande wa Mwekezaji, wote wameachia ngazi akiwemo mwenyekiti wao, Try Again, hivyo lazima iundwe safu mpya ya uongozi kuja kuungana na wajumbe upande wa wanachama wanaoendelea kudunda wakitangaza kwamba hawana mpango wa kujiuzulu kama wenzao.

IMANI YA MASHABIKI/WANACHAMA

Simba kufanya vibaya kwao imepelekea mashabiki na wanachama wa klabu hiyo kuondoa imani na timu yao kwamba itarudi kwenye ushindani kama zamani. Katika kipindi cha misimu mitatu sasa, Yanga imeendelea kutawala huku Simba ikisuasua na yote hayo lawama zinakwenda kwa viongozi.

Mo ametangaza kurejea, anapaswa kurudisha imani ya mashabiki na hilo haliwezi kufanikiwa kama itashindikana kuwa na timu nzuri. Simba ilikuwa ikisifika kwa kucheza soka la kuvutia, lakini hapo kati hali imebadilika, ikawa ni muhimu kupata ushindi tu, mengine ziada.

“Kiukweli tumepoteza falsafa yetu ya kucheza soka biriani, lazima turudi kwenye falsafa yetu,” anasema Mo.

KUIFUNGA YANGA NGAO YA JAMII

Watani wa jadi wa Simba ni Yanga, timu hizo zinapokutana hakuna ambaye anapenda kuona mwenzake ameshinda.

Hilo linaufanya mchezo wao kuwa na hisia kali sana ndani na nje ya uwanja. Msimu uliomalizika tulishuhudia timu hizo zikikutana mara tatu, mbili Ligi Kuu Bara na moja Ngao ya Jamii.

Katika Ngao ya Jamii, Simba iliibuka na ushindi kwa njia ya penalti baada ya muda wa kawaida kushindwa kufungana, wakabeba taji. Ndani ya ligi, Yanga ikatakata nje ndani kwa ushindi wa jumla wa mabao 7-2. Ile ya kwanza ilishinda 5-1, kisha 2-1.

Vipigo hivyo viliwauma sana Wanasimba kiasi cha kwamba viliondoka na makocha wao. 5-1 iliondoka na Roberto Oliveira ‘Robertinho’ na 2-1, Abdelhak Benchika akaondolewa.

Simba na Yanga zinakwenda kukutana tena katika mechi ya ufunguzi wa msimu ujao ambapo michuano hiyo inahusisha timu nne ikianzia nusu fainali. Zingine ni Azam na Coastal Union.

Nusu fainali itakuwa Yanga vs Simba na Azam vs Coastal Union, washindi wanakwenda fainali kuwania taji ambalo linashikiliwa na Simba. Hapa ni kipimo kingine cha Simba kuonyesha ubabe wao mbele ya Yanga na kutetea taji lao.

Wanasimba wanaamini kwamba uongozi uliopo madarakani ndiyo ulichangia pia kwa timu yao kuvurunda mbele ya Yanga katika msimu uliomalizika, hivyo kurejea kwa Mo matumaini kwao yamerudi upya. Kazi kwake.

BENCHI LA UFUNDI IMARA

Msimu uliomalizika, Simba imefundishwa na makocha watatu tofauti. Alianza Roberto Oliveira ‘Robertinho’, akaondoka Novemba 2023, akaja Abdelhak Benchikha ambaye naye safari iliishia Aprili 2024. Makocha wote hao ni wa kigeni, mzawa Juma Mgunda akamalizia.

Kitendo cha kubadilisha makocha ndani ya kipindi cha muda mfupi kimetajwa kuwa ni sehemu ya kufeli kwa Simba, hivyo Mo Dewji anapaswa kuliangalia hili.

“Tumeshindwa kutengeneza timu bora ya ushindani, eneo la benchi la ufundi halikuwa zuri hali ambayo imepelekea hata kupotea kwa falsafa yetu ya pira biriani. Hili ni eneo muhimu la kufanyia kazi. Nawaahidi nitashirikiana na viongozi wenzangu kusuka upya benchi la Ufundi,” amesema Mo.

UTAWALA WA SIMBA

Simba na Yanga ndiyo timu kongwe katika Ligi Kuu Bara na zimeweka utawala wao kwani katika kipindi cha misimu 20 iliyopita, zimekuwa zikibadilishana ubingwa wa ligi hiyo, mara moja tu Azam imeingilia kati.

Misimu mitatu mfululizo sasa, Yanga imeweka utawala wake kwa kubeba ubingwa wa ligi mfululizo, kabla ya hapo, Simba ilifanya hivyo kwa misimu minne nyuma.

Wakati Simba ikishinda ubingwa wa ligi mara nne mfululizo 2017/2018, 2018/19, 2019/20 na 2020/21, Mo Dewji alikuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, hivyo kuondoka kwake ni kama aliondoka na makombe yake.

KUCHEZA NUSU FAINALI CAF

Malengo ya Simba muda mrefu yalikuwa ni kucheza hatua ya nusu fainali katika michuano ya CAF, hiyo ni baada ya kucheza robo fainali mara tano kuanzia 2018. Misimu ya karibuni, timu hiyo katika kuishia kwao robo fainali ilionekana ni kitu kidogo tu kinawafelisha, hivyo kuelekea msimu ujao ambapo watashiriki Kombe la Shirikisho, wana kazi ya kufanya kufikia malengo.

UMOJA

Kauli mbiu ya Simba ni Nguvu Moja, lakini Mo Dewji anaamini kwamba umoja huo haupo kwa sasa, hivyo anaporejea katika kiti chake cha awali, anapaswa kulisimamia hilo ili kuonyesha kuna mabadiliko.

Mwenyewe amesema: “Tumekuwa hatupo wamoja hasa baada ya msuguano wa uchaguzi, malumbano na mgawanyiko umeendelea kutafuna timu yetu, hili jambo halina afya, naomba niwaombe Wanachama, Wanasimba na mashabiki tumalize tofauti zetu za uchaguzi na kuzizika kabisa kwa kauli yetu ya Simba ya Nguvu Moja.”

MCHAKATO WA MABADILIKO

Hapa ndiyo kuna kazi kubwa ya kufanya kwani tangu uanze mchakato wa mabadiliko ya uendeshaji wa Klabu ya Simba mwaka 2018, hadi leo kuna mvutano wa hapa na pale kiasi cha kufanya jambo hilo kuchelewa kukamilika.

Yamekuwa yakisemwa mengi juu ya mchakato huo wa mabadiliko, lakini jambo linalosubiriwa ni kuona kila kitu kikikamilika haraka kwani Wanachama wameridhia mabadiliko japo wanahitaji utaratibu ufuatwe.

Kuhusu mabadiliko, Mo anasema: “Nitahakikisha tunakwenda kukamilisha mchakato wa mabadiliko ya uendeshaji ili wanachama waweze pia kupata hisa zao stahiki na kuwa wamiliki wa Simba SC.”

SOKA LA VIJANA

Msingi wa timu nyingi zinazofanya vizuri kwa muda mrefu ni soka la vijana. Unaweza kuwa na timu bora kwa kununua wachezaji kila kipindi cha usajili lakini inaweza kufika wakati bajeti yenu inawabana hivyo wachezaji vijana mnaowakuza wanakuja kuwabeba.

Simba ni miongoni mwa timu ambazo huko nyuma zilikuwa na msingi mzuri wa soka la vijana. Tulishuhudia vijana wao wengi wakija kuwabeba mbele.

Hiyo ilitokea miaka ya 2012 hadi 2015, lakini baada ya hapo, ni kama wamejisahau, vijana wanaopandishwa timu ya wakubwa hawapewi ile nafasi ya kukua zaidi.

Hivi sasa kipa Ally Salim unaweza kusema ni mmoja kati ya vijana wao wanaopata hiyo nafasi, lakini ilipaswa wawepo vijana wengine wengi wanapewa nafasi kama ilivyokuwa miaka ya nyuma tuliposhuhudia Ramadhan Singano, Jonas Mkude, Said Ndemla na wengineo wakikiwasha.

MO amesema eneo hilo la uwekezaji kwa soka la vijana anakwenda kulisimamia kwa kuweka nguvu kubwa itakayozalisha vipaji kuanzia chini.

Chanzo: Mwanaspoti