Msemaji wa Klabu ya Yanga, Allly Kamwe amesema benchi la ufundi likiongozwa na kocha wake mkuu, Nasreddine Nabi tayari limeshawasoma wapinzani wao katika mchezo unaofuata wa kombe la Shirikisho Barani Afrika, Real Bamako ya Mali na tayari umeshaandaliwa mpango mkakati kwa ajili ya kuwakabili.
Kamwe amesema hayo alfajiri ya leo Alhamisi, Februari 23, 2023 wakati akiondoka na kikosi cha Yanga kuelekea Mali kwa ajili ya mchezo wa kundi D wa Kombe la Shirikisho Barani Afrika.
“Ni mchezo mhimu sana kwa Yanga kwenye safari yetu ya kuitafuta robo fainali, tunatafuta alama sita kwenye michezo hii miwili, wa ugenini na wa nyumbani, hata wachezaji wanajua, tunenda kucheza tukiwa na tahadhari kubwa ya kuepuka kupoteza.
“Lazima tupambane kuhakikisha tunapata alama tatu ugenini ama moja, maandalizi yako vizuri na tunaamini tuna nafasi ya kwenda kuvuna chochote ugenini.
“Tumewafuatilia Real Mamako, tunaenda Mali kuna watu wanaijua hiyo timu. Kipa wetu Diarra na beki wetu Mamadou Doumbia ni raia wa mali, wamecheza Stade Marien pale, wanaijua mitaa yote ya Bamako, mipango, ubora na udhaifu wao lazima tutumie faida ya kuwa na hawa watu kwenye timu yetu.
“Pia benchi la ufundi limefuatilia mechi zao zote kuanzia walipocheza na Mazembe, tuliwatazama tukiwa Tunisia.
“Mchezo wa pili dhidi ya Monastir tulikuwa kwenye mechi hapa na Mazembe lakini baadae benchi la ufundi walipata nafasi ya kurudia mechi ile kuitazama, kwa hiyo tumewasoma wanavyocheza nyumbani na ugenini ili kuweka mpango mkakati mzuri wa kuwakabili,” amesema Kamwe.
“Mechi yetu na Bamako hatuwezi kucheza kama tulivyocheza na TP Mazembe, hii ni mechi tofauti, tupo ugenini kwa hiyo na game plan itakuwa tofauti, lazima tuwe na tahadhari.
"Kwenye benchi la ufundi tunaye Profesa Nabi, huyu ni kocha haswa anayejua kucheza na kila aina ya mpinzani tunayekutana naye," amesema Ally Kamwe.
Katika Kundi D la Kombe la Shirikisho, US Monastir ya Tunisia wanaongoza wakiwa na alama 4, wakifuatiwa na Yanga wenye alama 3, TP Mazembe alama 3 na Real Bamako akivuta mkia na alama 1.