Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Prisons yazikataa 7 za Simba

Prisons Lake Tanganyika.jpeg Prisons yazikataa 7 za Simba

Mon, 4 Mar 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Msimu uliopita Tanzania Prisons iliingia kwenye rekodi ya kufungwa na Simba mabao 7-1, lakini sasa maafande hao wamegoma kuwa hawatakubali tena aibu hiyo, huku wakiahidi kucheza ‘man to man’ ili kuhakikisha wanalipa kisasi.

Prisons inatarajiwa kuwakabili Wekundu wa Msibazi keshokutwa, Jumatano katika mchezo wa Ligi Kuu utakaopigwa kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro ambao Wekundu ndio wenyeji, huku rekodi zikiibeba Simba dhidi ya wapinzani hao.

Akizungumzia mchezo wao na Simba, nahodha wa Prisons, Jumanne Elfadhir amesema wanafahamu ugumu watakaokabiliana nao, lakini kwa jinsi walivyoisoma Simba hawatambana mchezaji mmoja, bali ni kufa na yeyote.

Beki huyo mwenye mabao matatu na asisti moja aliyecheza mechi 17 kati ya 18 msimu huu ameongeza kuwa, “tutacheza ‘man to man’ kwa sababu Simba ina muunganiko mzuri ukimbana mmoja unaweza kuadhibiwa na mwingine.”

Amesema wanataka kuvunja uteja na kutokubali kufungwa idadi kubwa ya mabao kama ilivyokuwa katika mechi za mwisho walizokutana akiwaomba wenzake kuwa makini katika maeneo wanayocheza.

“Timu zote tumekuwa na matokeo mazuri katika michezo yetu ya mwisho. Hatuwezi kucheza kwa kumbukumbu (dhidi ya Simba), bali tunalenga ushindi na kuondoa uteja. Ile aibu iliyotukuta kwa sasa haijirudii,” amesema mchezaji huyo.

Katika mechi ya mwisho kukutana wapinzani hao, Prisons ikiwa nyumbani Sokoine Mbeya ilikunjwa mabao 3-1 huku msimu uliopita Wekundu wakiwa katika Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam walichapa mabao 7-1 katika mechi iliyopigwa Desemba 30, mwaka juzi.

Simba ambao wametoka kushinda mabao 6-0 dhidi ya Jwaneng Galaxy katika mchezo wa mwisho wa hatua ya makundi wa Ligi ya Mabingwa Afrika na kutinga robo fainali, wanajivunia rekodi ya kucheza mechi nane za Ligi Kuu bila kupoteza ikiwa ni sare tatu na ushindi mara tano.

Mara ya mwisho Wekundu hao kupoteza mechi ilikuwa Agosti 5 mwaka jana walipokandwa mabao 5-1 na watani zao Yanga, na tangu hapo hawajapoteza pointi tatu, ilhali wakiwa katika nafasi ya tatu na alama 36 kibindoni.

Kwa Prisons katika mechi nane wamepoteza moja dhidi ya Yanga kwa mabao 2-1 wakishinda tano na sare mbili, ambapo wanakamatia nafasi ya tano wakiwa na pointi 24 baada ya michezo 18 waliyocheza.

Chanzo: Mwanaspoti